Watu watatu wauawa na wanamgambo wa al- Shabaab, Kenya.
13 Januari 2020Vitengo tofauti tofauti vya polisi kwa sasa vinaendelea na msako wa kuwasaka magaidi waliovamia kituo kinachotoa huduma mbalimbali cha Kamuthe na kuwauawa walimu watatu na kumjeruhi mtoto mmoja katika tukio lililotokea majira ya saa nane usiku wa kuamkia leo.
Katika kisa hicho, wanamgambo hao pia waliharibu mtambo wa mawasiliano katika eneo hilo. Kulingana na mrakibu wa ukanda wa kaskazini mashariki Nicodemus Ndala, polisi inaendelea kuwasaka magaidi hao. Aidha, amewahakikishia walimu kuwa usalama wao utaimarishwa na hakuna haja ya kuyakimbia makaazi yao.
Ndala amesema "Nataka kuwapa Al-Shaabab na washirika wao onyo kali. Nilikuja hapa kutokana na tajriba yangu kwenye masula ya usalama kwa hivyo nitashirikiana na wenzangu ili kupambana na jinamizi hili na kulitokomeza kabisa. Kwa hivyo, nataka kuwahakikishia walimu, tutaendela kupambana na magaidi hadi tatizo hili litakapoisha kabisa.”
Wakati huo huo, viwango vya elimu katika jimbo la Garissa huenda vikashuka kutokana na mashambulizi ya magaidi kwenye eneo hilo.
Akizungumza kwa njia ya simu, katibu mkuu wa chama cha kutetea walimu KNUT tawi la Garissa, Abdirizak Hussein, amesema kuwa huenda walimu wanaofanya kazi katika eneo hilo wakaondoka kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Hussein amesema kuwa mashambulizi hayo yamekuwa yakiwalenga walimu na hilo litatiza hali ya masomo katika eneo la kaskazini mwa taifa. Hussein anafafanua zaidi. "Shule zitafungwa kwa sababu walimu na wanafunzi wote wamekimbia. Maisha sasa si nzuri na tayari shule fulani imefungwa na hii pia naona itafungwa.”
Shambulio hilo la leo linajiri wiki moja tu baada ya wanamgambo hao kushambulia shule ya msingi ya Saretho katika jimbo hilo la Garissa na kuwauwa wanafunzi wanne.
Tangu mwezi Desemba mwaka uliopita, kundi hilo la kigaidi limeongeza mashambilizi yake nchini Kenya ikiwemo uvamizi wa kambi ya jeshi kwenye eneo la Manda katika jimbo la Lamu.
Hili ni shambulizi la tatu ambalo limefanywa na kundi hilo la kigaidi ndani ya mwezi huu wa Januari. Hii sio mara ya kwanza kwa walimu katika jimbo hilo la Garissa kuvamiwa na kuuwauwa. Miaka miwili iliyopita, walimu wawili waliuawa na kusababisha walimu wengine ambao hawakuwa wenyeji wa eneo hilo kukimbia kutoka eneo pana la kaskazini mashariki wakihofia usalama wa maisha yao.