Algeria yasubiri matokeo ya uchaguzi wa rais
7 Septemba 2024Matangazo
Zoezi la kupiga kura lilianza mapema saa mbili asubuhi saa za Algeria na lilihitimishwa saa kumi na moja jioni. Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutolewa kesho Jumapili.
Rais aliye madarakani Abdelmadjid Tebboune anatazamiwa kushinda muhula wa pili madarakani akiwashinda wapinzani wawe wawili. Wanaochuana naye ni Abdelaali Hassani anayegemea siasa za dini ya kiislamu na mgombea wa kambi ya wasoshalisti Youcef Aouchiche.
Tebboune aliingia madarakani Disemba mwaka 2019 kiasi mwaka mmoja baada ya maandamano ya umma kumlazimisha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika kujiuzulu. Anatumai safari hii raia wengi watajitokeza kupiga kura kufuatia idadi ndogo ya wapigakura katika uchaguzi uliopita.