Algeria yatuma maombi kujiunga na kundi la BRICS
22 Julai 2023Taarifa hizo zimeripotiwa na kituo cha televisheni cha nchini Algeria cha Ennahar kikimnukuu rais Abdelmadjid Tebboune. Chombo hicho kimesema rais Tebboune alizungumzia suala hilo alipokuwa akihitimisha ziara yake nchini China mwishoni mwa wiki hii, ambapo alisema Algeria inataka kujiunga na kundi la BRICS kwa lengo la kufungua fursa mpya za kiuchumi.
Soma zaidi:BRICS yajadili uwezekano wa kujitanua na kujumuisha nchi zinazosafirisha mafuta
Taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika lina utajiri mkubwa wa mafuta na gesi asili na limekuwa likijaribu kuimarisha sekta nyingine za kiuchumi kupitia ushirika na mataifa makubwa mfano wa China.
Kundi la BRICS linaloyajumuisha mataifa ya China, Brazil, India, Urusi na Afrika Kusini linazingatiwa kuwa mbadala wa makundi mengine ya ushirkiano ya kiuchumi yanayotawaliwa na mataifa ya magharibi.