Amerika Kusini yaipiku Ulaya kwa vifo vya COVID-19
5 Agosti 2020Sasa Amerika ya Kusini imefikisha asilimia 30 ya vifo vyote vilivyotokea duniani kutokana na virusi vya korona baada ya jioni ya jana kufikisha vifo 206,000.
Brazil, taifa ambalo limeathirika zaidi na janga hilo, ilikuwa imeripoti vifo 95,819 kufikia jioni ya jana.
Watu 1,154 walikufa jana pekee. Jumla watu milioni 2 na laki nane wamegundulika na virusi vya korona nchini humo.
Leo hii, waziri kwenye ofisi ya rais, Jorge Oliveira, amekuwa mjumbe wa nane wa baraza la mawaziri la Rais Jair Bolsonaro kuambukizwa maradhi hayo ya COVID-19.
Mwenyewe, Rais Bolsonaro na mkewe, Michelle, pia walishaupata ugonjwa huo, lakini sasa kiongozi huyo anayefuata siasa kali za mrengo wa kulia, ameanza tena kazi baada ya vipimo vya mwisho mwishoni mwa mwezi uliopita kuonesha kuwa hana tena maambukizo.
Mexico, ambayo ni ya pili kwenye eneo hilo, imeripoti vifo 48,869 hadi sasa. Wizara ya Afya ya Mexico inasema watu zaidi ya 6,000 waligunduliwa kuambukizwa virusi vya korona ndani ya kipindi cha masaa 24 tu yaliyopita, huku wengine 857 wakipoteza maisha ndani ya kipindi hicho.
Mexico ina jumla ya watu laki 4 na nusu walioambukizwa na tayari imeshapoteza takribani 49 alfu miongoni mwao.
Marekani yaendelea kushika nafasi ya kwanza
Marekani, kwa upande wake, imeongeza watu wengine wapatao 54,000 kwenye orodha ya maambukizo mapya, na vifo vipya 1,302 ndani ya masaa 24 yaliyopita, kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha John Hopkins.
Hadi kufikia jioni ya jana, Marekani ina watu milioni 4,765,170 walioambukizwa virusi hivyo, na imeshawapoteza 156,668 miongoni mwao, na kuifanya nchi inayoongoza duniani.
Hata hivyo, Rais Donald Trump anasema kupatikana kwa idadi hiyo ni kwa sababu serikali yake imeamuwa kuwapima watu wengi kadiri inavyowezekana kuliko nchi nyengine yoyote duniani.
Hapa barani Ulaya, Ufaransa na Uholanzi zimeanza kutayarisha kanuni za kulamisha utekelezwaji wa hatua za kinga dhidi ya virusi hivyo, katika wakati ambapo vifo duniani vimegonga laki 700,000.
Miji ya Paris na Toulouse imetangaza kwamba kuvaa barakowa ni jambo la lazima hasa kwenye mitaa yenye watu wengi.
Nchini Uholanzi, hatua kama hizo zilianza kutekelezwa Jumatano (Agosti 5) kwenye miji ya Amsterdam na Rotterdam.
Kwa upande wake, Ireland imeahirisha kufunguwa baa na klabu za usiku kutokana na ushauri wa wanasayansi wake.