Kamala Harris aanza kampeni za Urais
22 Julai 2024Chama cha Democratic nchini Marekani kimeanza mbio za kuteua atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi ujao mwezi Novemba baada ya Rais Joe Biden kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho jana Jumapili na kumpendekeza makamu wake Kamala Harris kupambana na Donald Trump wa Republican.
Mengi yameendelea kuzungumzwa kufuatia hatua hiyo ya Biden, ambaye alikabiliwa na shinikizo kubwa hivi karibuni la kujiengua kutokana na wasiwasi uliozidi kuhusiana na uwezo wake wa kuongoza.
Mgombea wa chama cha Republican na aliyetarajiwa kupambana na Biden kwenye uchaguzi wa Novemba, Donald Trump, alikuwa miongoni mwa viongozi wa mwanzo kutoa maoni yao kufuatia hatua hiyo. Trump aliandika kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social kwamba Joe Biden "hakupaswa kugombea" muhula wa pili. Hakuachia hapo, bali pia alihoji uwezo wake katika muda uliosalia. Biden amesema, ingawa anajitoa lakini bado atabakia White House hadi mwishoni mwa uongozi wake Januari 20, 2025.
Soma pia:Biden aapa kushinda pamoja na kushinikizwa asishiriki uchaguzi wa Novemba
Wabunge na wazee wa chama hicho, ikwia ni pamoja na karibu theluthi ya maseneta, magavana wenye ushawishi wametoa matamko yao kufuatia hatua hiyo.
Obama, Pelosi wajizuia kuzungumzia uteuzi wa Harris
Bill Clinton, Rais wa zamani wa Marekani pamoja na mkewe Hillary, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya kigeni chini ya Rais Barrack Obama, wamekwishatangaza kumuunga mkono Kamala Harris.
Lakini, majina makubwa kuanzia kiongozi wa walio wachache bungeni Hakeem Jeffries, Spika aliyemaliza muda wake na mwenye ushawishi mkubwa Nancy Pelosi, hadi kiongozi wa walio wengi katika Baraza la Seneti Chuck Schumer na Rais wa zamani Barack Obama, wamejaribu kujizuia kusema lolote kuhusiana na hatua hiyo ya kumuidhinisha Harris, ingawa walimpongeza Biden kwa kujiengua.
Soma pia: Shinikizo la kumtaka Biden kutowania muhula wa pili laongezeka
Taarifa ya Obama ilisema tu kwamba watafuatilia mwenendo katika siku zijazo, na kuongeza kuwa ana imani kubwa kwamba viongozi wa chama chake cha Democratic wataweza kuanzisha mchakato utakaoibua mgombea imara.
Soma pia:Trump: Nagombea kuwa Rais wa Marekani yote
Harris aanza kampeni mara moja
Harris, hakuchelewa kuanzisha kampeni ya urais mara baada ya kuidhinishwa na Biden akiwaomba Wademocrats wenzake kumuunga mkono. Maafisa kwenye kampeni yake walianza mara moja kuwapigia simu wajumbe wa mkutano huo mkuu wa chama mwezi ujao wakijaribu kuwashawishi kumuunga mkono mwanamama huyo ambaye huenda akawa wa kwanza kushika wadhifa huo katika historia ya Marekani.
Shirika la habari la Reuters liliripoti likinukuu vyanzo mbalimbali kwamba wenyeviti wote 50 wa majimbo wa chama hicho watamuunga mkono Harris.
Duru zenye uelewa na suala hilo zimesema, Harris, alizungumza na Gavana wa Pennysilvania Josh Shapiro, ambaye huenda akawa mgombea mwenza, kiongozi wa chama hicho bungeni Hakeem Jeffries pamoja na mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Weusi, Steven Horsford.
Kiongozi wa walio wengi katika Baraza la Seneti Chuck Schumer, aliyeusifu uamuzi wa Biden wa kuachia ngazi pia hakusema chochote kuhusiana na mgombea ajaye wa chama hicho. Seneta wa kwanza wa Democrats kuanza kumtaka Biden kujiuzulu, Peter Welch yeye alitoa tu wito wa uwazi katika mchakato wa kumpata mgombea.
Mgombea atakayechukua nafasi hiyo ya Biden anatarajiwa kutangazwa katika mkutano mkuu wa Democrats mnamo Agosti 19.