Baraza kuu la UN mbioni kuanza
24 Septemba 2018Viongozi takriban 130 wa taifa na serikali wanatarajiwa kuwasili wiki hii mjini New-York kuhudhuria hadhara kuu ya Umoja wa mataifa- kongamano linalozungumzia migogoro inayoikumba sayari yetu na ambako makubaliano kufikiwa pembezoni mwa mikutano.
Viongozi wa mataifa 193 wanachama wa Umoja wa mataifa wanawakilishwa katika hadhara kuu. Rais wa Marekani Donald Trumpo, sawa na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa watahudhuria huku wengine mfano wa kansela Angela Merkel wa Ujerumani, au Vladimir Putin wa Urusi watawakilishwa na mawaziri wao wa mambo ya nchi za nje. Haijulikani bado kama rais wa Venezuela Nicolas Maduro atahudhuria mkutano huo au la.
Mada moto moto safari hii mjini New York ni pamoja na mvutano wa Marekani pamoja na Iran, kujitoa Marekani katika mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi , Korea ya Kaskazini, na mvutano kati ya Israel na Palestina.
Rais wa Marekani Donald Trump anaehudhuria kwa mara ya pili baada ya kuingia ikulu ya mmarekani amepangiwa kuhutubia kesho jumanne.Tayari ameshawasili mjini New York ambako jana usiku alizungumza na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na kuzungumzia kuhusu Korea ya Kaskazini ,masuala ya ulinzi na biashara miongoni mwa mengineyo.
Mbali na viongozi wa mataifa wanachama , hadhara kuu ya Umoja wa mataifa, limegeuka jukwaa muhimu kwa mashirika yasiyomilikiwa na serikali kuitisha pia mikutano yake, kuendeleza warsha, mijadala na maonyesho ya utamaduni yanayowavutia watu kadhaa mahuhuri. Waandishi habari zaidi ya 3000 kutoka kila pembe ya dunia wanahudhuria hadhara kuu na mwaka huu .
Kuanzia kesho jumanne wawakilishi wa kila nchi wataanza kupanda jukwaani kuanzia saa tatu asubuhi hadi tatu usiku kuhutubia kwa lugha tofauti.
Polisi mjini New-York imewekwa katika hali ya tahadhari na kuligeuza eneo yanakokutikana makao makuu ya Umoja wa mataifa katika fukwe za East River kuwa ngome.Mamia ya polisi tangu waliovalia sare mpaka waliovalia kiraia wamewekwa juu ya mapaa ya nyumba au ndani ya meli katika East River.
Na saamu la Nelson Mandela limefunuliwa leo kataika Umoja wa mataifa ili kuadhimisha amiaka 100 tangu kiongozi wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini,Nelson Mandela alipozaliwa.Akizungumza katika hafla hiyo katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amemtaja"Nelson Mandela kua kitambulisho cha maadili ya umoja wa mataifa, ya amani, hali ya kesameheana, huruma na utu.
Mkutano wa kilele kuhusu amani umepangwa kuitishwa baadae hii leo kwa hishma ya Nelson Mandela.Mwenyekiti wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa Maria Fernanda Espinosa amesema anataraji sanamu hilo litawapa moyo viongozi wa mataifa wanachama na kuwakumbusha "tofauti zilizoko zinaweza kusherehekewa."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman