Adama Barrow kuapishwa Januari 19 kama ilivyopangwa
16 Januari 2017Msemaji huyo amesisitiza kuwa hakuna mabadiliko yoyote kwa kusema kuwa utawala wa Jammeh utakamilika Januari 19 siku ambayo rais mteule Barrow ataanza rasmi awamu yake ya uongozi. "Ataapishwa na atachukua ofisi tarehe hiyo hiyo bila kushindwa" alisema Mai Fatty
Sherehe za kuapishwa zinatarajiwa kufanyika Januari 19 lakini rais anayemaliza muda wake Yahya Jammeh, anapinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Disemba 1 mwaka jana katika mahakama ya juu nchini humo.
Shirika la habari la APS limemnukuu rais wa Senegal Macky Sall akisema kuwa, amekubali kumpokea Barrow katika nchi yake kufuatia ombi la nchi wanachama wa jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Maghabiri, ECOWAS, makubaliano ambayo yalifikiwa katika mkutano wa viongozi wa Ufaransa na Afrika uliofanyika katika mji mkuu wa Mali, Bamako.
ECOWAS iliiweka Alhamisi wiki iliyopita kuwa ndio tarehe ya mwisho ya kujaribu kutatua mgogoro wa kisiasa nchini Gambia, radio ya kimataifa ya Ufaransa RFI ilimnukuu rais wa Togo Faure Gnassingbe akisema, kitendo cha Jammeh kukataa kukubali kushindwa kinachochea hofu ya kuwepo kwa machafuko katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Rais mteule Barrow alihuduria mkutano huo wakati Jammeh hakuhudhuria, mkutano huo unafuatia mazungumzo kati ya wapatanishi wa ECOWAS na viongozi hao wawili yaliyofanyika nchini Gambia.
Taarifa kutoka katika ofisi ya rais mteule Barrow inasema kuwa mkutano kati ya rais Jammeh, rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na wawakilishi wengine wa ECOWAS haukuwa na matokeo mazuri.
Mazungumzo ya ECOWAS yalianza saa kadhaa baada ya chama kikuu cha upinzani nchini Gambia kufungua mashitaka katika mahakama ya juu kupinga kuapishwa kwa rais mteule Januari 19.
Awali ECOWAS iliahidi kutuma vikosi nchini Gambia kuhakikisha kuwa kunakuwa na kubadilishana madaraka kwa amani, iwapo Jammeh ataendelea kushikilia msimamo wake wa kukataa kuachia madaraka baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa zaidi ya miongo miwili.
Mwandishi: Celina Mwakabwale/DPA/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga