Benzema ashinda tuzo ya "Ballon d´Or"
17 Oktoba 2022Mshambuliaji wa Ufaransa Karim Benzema ndiye mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa soka duniani "Ballon d'Or". Benzema alitangazwa Jumatatu usiku katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Théatre du Chatelet mjini Paris.
Ushindi huo unajiri baada ya kiwango chake kizuri kuisaidia Real Madrid kushinda Ligi ya Mabingwa na La Liga msimu uliopita. Benzema, ambaye ni mshindi wa kwanza wa Ufaransa wa tuzo ya kifahari zaidi ya mtu binafsi katika soka tangu Zinedine Zidane mwaka 1998, alifunga mabao 44 katika michezo 46 katika klabu yake ikiwa ni pamoja na 15 katika Ligi ya Mabingwa.
Benzema mwenye asili ya Afrika, amewapiku Sadio Mane wa Bayern Munich na Senegal, Kevin de Bruyne wa Manchester City na Ubelgiji na Robert Lewandowski wa Barcelona na Poland ambao wamekuwa wakiwania pia tuzo hiyo.
Mane na Lewandowski hawakuondoka patupu
Hata hivyo nyota wa Senegal na Bayern Munich Sadio Mane amejishindia kwa mara ya kwanza tuzo ya "Socrates" kutoka kwa waandaaji wa France Football. Tuzo hiyo imepewa jina la kiungo wa zamani wa Brazil, na inakusudiwa kubainisha "mpango bora wa kijamii" kwa wachezaji wanaojitolea nje ya uwanja ili kusaidia wengine, na kwa upande wa Mane wametambua kazi ambayo ameifanya kwa jamii katika nchi yake.
Kwa upande wake Robert Lewandowski hakuondoka mikono mitupu, amejishindia tuzo ya mfungaji bora maarufu kama "Gerd Müller". Alipokuwa akiipokea tuzo hiyo, Didier Drogba alimtania kuwa mwakani huenda akawa na kibarua kigumu kutwaa tuzo hiyo hasaa ukizingatia kasi wanayokuja nayo wachezaji chipukizi kama Erling Haaland, lakini Lewandoski amesema bado yupo ngangari na hajatoa kauli yake ya mwisho.
Gavi na Courtois watunukiwa
Pablo Martin Paez Gavira maarufu "Gavi" wa Barcelona mwenye umri wa miaka 18 amejishindia tuzo ya mchezaji-chipukizi maarufu kama "Copa" huku mlinda lango wa Ubelgiji na Real Madrid Thibaut Courtois akijishindia tuzo ya Golikipa bora. Ilikuwa fursa pia ya kumuona mchezaji Sebastien Häller ambaye anasumbuliwa na saratani, huku akitaja kuwa kwa sasa hali yake inaendelea kuimarika.
Alexia Putellas wa Uhispania na mchezaji wa Barcelona alitunukiwa kwa mwaka wa pili mfululizo tuzo ya Ballon d´Or kwa upande wa wanawake. Timu bora iliyochaguliwa katika hafla hiyo ni Manchester City yake Kevin De Bruyne.
Tuzo ya Ballon d'Or ambayo hutolewa na jarida la France Football kwa wachezaji wa kiume tangu mwaka 1956, aliposhinda Stanley Matthews alishinda. Tuzo la wanawake liliundwa mnamo mwaka 2018, na zote mbili zilighairishwa mwaka 2020 kutokana na janga la Covid. Kwa mara ya kwanza mwaka huu, tuzo ya Ballon d'Or imetilia maanani mafanikio ya msimu uliopita tofauti na ilivyo kawaida.