Binti wa dos Santos anakabiliwa na kesi mahakamani
6 Januari 2020Marais wa Angola na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wamemtaka binti wa rais wa zamani wa Angola, Isabel dos Santos na mumewe Sindika Dokolo kushirikiana na mahakama baada ya mali zao kuzuiwa na serikali. Katika taarifa yao Rais wa Angola, Joao Lourenco na Rais wa Congo, Felix Tshisekedi wamesema njia bora ya kuweza kusonga mbele na upelelezi ni dos Santos, Dokolo pamoja na Mario Leite da Silva, mwenyekiti wa benki ya maendeleo ya Angola, BFA, kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika za serikali na mahakama ya Angola. Marais hao walikutana jana kwenye mji wa Angola, Benguela. Taarifa ya mahakama iliyotolewa Desemba 23 inaeleza kuwa serikali inaamini dos Santos na mumewe Dokolo, raia wa Kongo pamoja na Silva wanatuhumiwa kwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya dola bilioni moja. Dos Santos na mumewe wamekanusha madai dhidi yao wakisema yanachochewa kisiasa.